Lishe bora ni kula chakula cha kutosha na chakula kinachofaa ili kiweze kusaidia mwili kukua vyema kwa afya njema na kuweza kupigana na magonjwa mwilini pia Utapiamlo ni lishe mbaya na hutokea ikiwa unakula chakula kidogo sana au kingi sana au kula chakula kisichokuwa na lishe ya kutosha.
Miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula Tanzania ni pamoja na Mkoa wa Ruvuma, licha ya ongezeko hilo la chakula bado kumekuwepo na tatizo la utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano.
Tathimini ya utekelezaji wa kamati ya lishe Manispaa ya Songea kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2021 kiwango cha watoto wenye utapiamlo kimepanda kutoka asilimia 0.1% Oktoba hadi Disemba 2020 na kufikia asilimia 0.2% Januari hadi Machi 2021 ambapo jumla ya watoto 24 kati ya watoto 37,502 waligundulika kuwa na utapiamlo mkali ukilinganisha na kipindi cha Robo mwaka iliyopita Oktoba hadi Disemba 2020 ambapo watoto 21 kati ya watoto 36,748 wenye umri chini ya miaka mitano waliogundulika kuwa na utapiamlo.
Ongezeko hilo la watoto wenye utapiamlo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2021, ni kutokana na baadhi ya wazazi kujishughulisha na shughuli za kilimo kwa kipindi cha masika ya mvua na kuacha watoto bila chakula cha kutosha kwenye kaya zao.
Hayo yameelezwa na kamati ya lishe Manispaa ya Songea kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa zoezi la lishe katika kipindi cha Robo mwaka Januari hadi Machi 2021 iliyofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya leo tarehe 3 Mei 2021.
Wakibainisha baadhi ya changamoto zinazopelekea ongezeko la watoto wenye utapiamlo wenye umri chini ya miaka mitano ni pamoja na uhaba wa chakula dawa (RUTF) katika vituo vya Afya na baadhi ya watoa huduma katika vituo vya Afya kutokuwa na uelewa juu ya elimu ya lishe.
Ili kukabiliana na changamoto hizo Manispaa ya Songea imejipanga kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara, kuundwa kwa kamati za lishe mashuleni, Wataalamu wa Afya kuelimisha namna ya uandaaji wa lishe bora kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kuhakikisha akina mama wajawazito wanahudhuria kliniki mara anapohisi ana ujauzito, Kutumia sheria ndogo za lishe, watendaji wa kata/ mtaa kufuatilia kaya zenye watoto wenye utapiamlo, kuhakikisha kila shule inatengeneza bustani za mboga mboga na kupanda miti ya matunda, pamoja na kutolewa kwa mafunzo maalumu ya uandaaji wa chakula cha lishe kwa wanafunzi mashuleni.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA,
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.