Kijiji cha Litembo, kilichoko wilayani Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma, si tu sehemu ya mandhari ya kuvutia na ya asili,bali ni ukurasa hai wa historia ya ushujaa na mapambano ya kabila la Wamatengo dhidi ya ukoloni wa Kijerumani.
Ni hapa ambapo historia inazungumza kupitia jiwe kubwa linalofanana na kichwa cha tembo, jiwe lililopewa jina la Litembo, na kuwa kitovu cha kumbukumbu ya mashujaa 800 waliouawa kikatili Machi 4, 1902.
Jiwe la Litembo si jiwe la kawaida. Likiwa limejengwa kwa maumbile ya ajabu ya kiasili, linabeba simulizi nzito ya mauaji ya kikatili yaliyofanywa na wakoloni wa Kijerumani dhidi ya Wamatengo waliokataa kwa dhati kutawaliwa.
Ndani ya jiwe hilo, kuna pango refu linalosemekana kupita chini ya ardhi kutoka Litembo hadi Kijiji cha Maguu,pango ambalo liliwasaidia mashujaa wachache walionusurika kuokoa maisha yao.
Pango hilo linaaminika kuwa na wanyama wakali, nyoka, maji mengi, na hata madini ya thamani. Kwa wakazi wa eneo hilo, ni si tu maficho ya vita, bali pia ni hazina ya ajabu.
Vita ya Haki Dhidi ya Bunduki 19
Mnamo mwaka 1902, kiongozi wa kijerumani aliyejulikana kwa jina la Korongo alitaka kuwafanya Wamatengo kuwa chini ya himaya yake.
Alituma ujumbe kwa viongozi wa jadi, akiwataka wamsaidie,lakini majibu hayakuwa alivyotarajia. Kwa kushirikiana, viongozi hao walikusanya watu wao kwa kupiga ngoma kubwa na kutoa uamuzi wa kishujaa: “Hatutatawaliwa.”
Hasira ya mkoloni ikafuatia. Korongo alikuja na wapiganaji wake waliobeba bunduki 19,silaha dhidi ya mikuki, mishale na mapanga.
Lakini mashujaa wetu hawakuogopa. Walijipanga nyuma ya jiwe la Litembo, na mapigano makali yakaanza.
Hapo ndipo damu ya mashujaa 800 wa Wamatengo ilimwagika kwenye ardhi yao, wengine wakidai waliona damu hiyo ikiingia kwenye mto Mapipa hadi ziwa Nyasa.
Makaburi ya Heshima na Mnara wa Kumbukumbu
Mashujaa hao walizikwa kwa heshima kubwa, japo kwa uchungu. Kila kaburi linahifadhi mashujaa zaidi ya 25, yote yakiwa ndani ya kijiji hicho hicho cha Litembo.
Ili kuenzi historia hiyo, mnara wa makumbusho umejengwa karibu na jiwe la Litembo, ambapo kila mwaka tarehe 28 Novemba, hufanyika maadhimisho ya kuwakumbuka mashujaa hao.
"Ni siku ya machozi na fahari," anasema Bruno Tembo, Katibu wa Baraza la Mila na Utamaduni Kata ya Litembo. “Tunawakumbuka wazee wetu waliotoa maisha yao kwa ajili ya uhuru kabla hata ya taifa kuitwa Tanganyika.”
Fursa ya Utalii wa Kishujaa
Kwa upande mwingine, Serikali ya Mkoa wa Ruvuma imeona thamani ya kipekee ya eneo hili si tu kihistoria, bali pia kama kivutio cha utalii.
Afrikanus Challe, Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa, anasema juhudi zinaendelea kulitangaza Litembo kimataifa, ili wageni wengi waje kushuhudia ushahidi wa mapambano ya kweli ya ukombozi dhidi ya wakoloni.
"Hatuzungumzii historia kwenye vitabu tu, hapa Litembo historia iko hai. Unashika jiwe lililolowa damu ya mashujaa, unatembea kwenye pango walilotumia kuokoa maisha yao. Ni hadithi ya kweli ya ushujaa wa Kiafrika,” anasema Challe kwa msisitizo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.