TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inafanya mazoezi mawili ya uwekaji wazi na uboreshaji wa daftari la kudumu la Mpigakura katika Jimbo la Uchaguzi la Songea mjini kuanzia Mei 2 hadi 4 mwaka huu.
NEC Jimbo la Songea mjini tayari imetoa mafunzo kwa kuzingatia miongozo ya kujikinga na virusi vya corona kwa waandishi wasaidizi na BVR KIT OPERATORS wapatao 42 watakaofanya kazi katika kata 21 za Manispaa ya Songea.
Walioteuliwa kufanya kazi hiyo wamekula kiapo na kupata Mafunzo ambayo yametolewa kwa siku moja kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea na kufunguliwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Philipo Beno.
Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo,Beno amewatahadharisha wote walioteuliwa kufanyakazi ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili katika kata zote 21 za Manispaa hiyo kuchukua tahadhari kwa kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya virusi vya corona.
“Kwa kuwa ninyi ndiyo wasimamizi hakikisheni kila anayekuja anaosha mikono kwa maji tiririka na sabuni na pia avae barakoa kwa sababu hivi sasa barakoa zipo za kutosha,wewe utakuwa naye kwa karibu wakati mnafanya mahojiano kwa hiyo wewe utakuwa umejikinga na yeye atakuwa amejikinga’’,amesisitiza Beno.
Nuru Riwa ni Afisa wa Tume Idara ya Habari na Elimu ya Mpigakura amesema Tume ya Uchaguzi imenunua vifaa vyote muhimu vya kujikinga na virusi vya corona vikiwemo barakoa,vitakasa mikono,ndoo za maji,sabuni,mipira ya kuvaa mikononi na sipiriti ambapo amewaasa walioteuliwa kufanyakazi hiyo kuhakikisha wanavitumia ipasavyo vifaa ili kujikinga na corona wakati wanatekeleza majukumu yao.
“Utakapokuwa vituoni ili usichukue wala kusambaza virusi vya corona ni lazima ujikinge,tumia vifaa vyote ulivyopewa kwa sababu corona ni hatari,lengo ni kwamba unapomaliza ili zoezi usipokee maambukizi wala kuwaambukiza wengine’’,alisisitiza Riwa.
Amesema zoezi hilo katika Manispaa ya Songea linatarajia kufanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 2 hadi 4,2020 na kwamba yanafanyika mazoezi mawili ambayo ni uwekaji wazi wa daftari la kudumu la mpigakura na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Kwa mujibu wa Afisa huyo, zoezi hilo japo linatumia siku tatu ni zito kwa sababu linafanyika katika mwaka wa uchaguzi Mkuu na kwamba mazoezi haya kabla ya uchaguzi yanafanyika Tanzania bara ya visiwani.
Ameitaja mikoa inayohusika katika mazoezi hayo kwa upande wa Tanzania bara kuwa ni Ruvuma, Njombe, Lindi, Mtwara, Dodoma,Singida,Rukwa,Mbeya,Morogoro,Iringa,Dar es salaam na Pwani na kwamba Tanzania visiwa ni ni Unguja na Pemba.
“Katika mazoezi haya ya uwekaji wazi daftari la wapigakura na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya pili tunaanza tarehe 2/5/2020 hadi 4/5/2020,tunaomba wananchi kujitokeza ili kuhakiki taarifa zake,orodha ya majina ya wapigakura itabandikwa kila kituo’’,alisema.
Hata hivyo ametoa rai kwa wananchi wanapofika kwenye vituo hivyo kuzingatia tahadhari za afya dhidi ya virusi vya corona na kwamba inashauriwa katika familia moja kumchagua mtu mmoja kuhakiki taarifa za wengine ili kuepukana na mkusanyiko ambao ni hatari kuambukizwa na corona.
Adamu Mkina ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango,Tume ya Taifa ya Uchaguzi,Idara ya Mipango,Ufuatiliaji na Tathmini amesema katika zoezi hilo mfumo utafunguliwa ndani ya kata husika.
Ametoa rai kwa wananchi watakaokuwa wanafika kuhakikiwa katika zoezi hilo kujua Mtaa au kijiji anachotoka ili kuwarahisishia walioteliuwa kufanya kazi hiyo ya kitaifa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 30,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.