HOTELI YA MBICU MBINGA KUWA NA HADHI YA KIMATAIFA
CHAMA Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Mbinga Nyasa (MBIFACU) mkoani Ruvuma kimeanza mradi wa ukarabati wa hoteli ya MBICU ambayo inamilikiwa na chama hicho ili iweze kuwa na viwango vya kimataifa.
Kaimu Meneja wa MBIFACU Henrick Ndimbo amesema ukarabati wa hoteli hiyo ambao umeanza mwaka wa fedha wa 2019/2020 unatarajia kukamilika baada ya miaka mitatu na kwamba katika kutekeleza mradi huo zaidi ya shilingi bilioni moja zitatumika.
Hata hivyo amesema ukarabati wa hoteli hiyo unafanyika kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza yanajengwa majengo sita na kujenga uzio ambao utazunguka eneo lote la hoteli hiyo.
“Eneo hili litakuwa majengo 15 pamoja na jengo la hoteli,majengo yote yataezuliwa na kuezekwa katika mtindo wa kisasa ili kukidhi viwango vya kimataifa na kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi’’,alisisitiza Ndimbo.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa MBIFACU Winfred Lupembe amesema mara baada ya kukamilisha mradi huo wanatarajia kuongeza mapato makubwa kupitia hoteli ya MBICU ambayo wageni watakuwa wanapata malazi, chakula na hudumu nyingine.
Henrick Ndimbo/Kaimu Meneja MBIFACU
Amesema kutokana na hoteli hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa wanatarajia kupokea wageni wa kimkoa,kitaifa na kimataifa na kwamba Bodi ya chama hicho imefanikiwa kusimamia shughuli za ukarabati wa hoteli hiyo ambazo zinaendelea vizuri na wanatarajia kukamilisha kwa wakati.
Bumi Masuba ni Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Ruvuma anasema kuwa hoteli ya MBICU ilijengwa miaka ya 1990 na kwamba ilisimama kutoa huduma kutokana na ubovu wa miundombinu yake.
Hata hivyo amesema MBIFACU wameamua kuifanyia ukarabati mkubwa hoteli hiyo na mara baada ya ukarabati kukamilika hoteli ya MBICU itakuwa ni miongoni mwa hoteli bora zaidi katika Mkoa wa Ruvuma.
“Hoteli hii itakuwa ni ya kipekee katika Mkoa wa Ruvuma kwa sababu mgeni atapata mahali pa kulala,kula,kunywa,bustani maarufu ya kupumzikia,eneo la kuegesha magari,hii ni hoteli yenye eneo kubwa sana ina kila kitu,hapa itakuwa ni zero grazing’’,alisisitiza Masuba.MBIFACU ni Chama cha Ushirika ambacho kilianzishwa Agosti mwaka 2000 na kinafanya shughuli zake katika wilaya za Mbinga na Nyasa,chama hicho pia kinatoa huduma kwa wakulima wanaolima kahawa wilaya ya Songea. songeamc.go.tz
Picha chini ukarabati wa majengo mapya ya hoteli ya MBICU
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 5,2020
Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.