Mbinga. Katika kipindi cha siku tatu tuu Halmashauri ya Mji wa Mbinga imefikia asilimia 80.4 ya lengo la kuwapatia kinga tiba ya usubi wakazi 126,866 ndani ya siku saba.
Usubi ni ugonjwa unaoathiri ngozi na macho ambapo husababisha ngozi kuwasha sana na kuwa ngumu kama mamba, kenge au mjusi na yenye madoadoa kama chui na bila matibabu hupelekea upofu.
Vimelea vya ugonjwa huu huenezwa na nzi wadogo weusi wanaopatikana katika mito inayoenda kwa kasi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Dkt Kung'e Nyamuryekung'e alisema waliopatiwa kinga tiba mpaka leo Agosti 19 ni watu 102,016.
Ili kusema zoezi la kinga tiba ya usubi limefanikiwa inatakiwa kumezesha dawa walau asilimia 80 ya wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga kati ya Agosti 17 zoezi lilipoanza na Agosti 23 siku litakapotamatika.
Tafsiri ya kufikia asilimia 80.4 ya lengo siku ya tatu baada ya zoezi kuanza ni kwamba kuna uwezekano mkubwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga ikafikia na hata kuzidi lengo kabla ya siku saba zilizopangwa kumalizika.
"Zoezi linakwenda vizuri. Mwitiko wa wananchi ni mkubwa tofauti na miaka ya nyuma," alisema Dkt Nyamuryekung'e.Kwa muda mrefu usubi, ugonjwa maarufu kama River blindness, umekuwa moja ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele na umekuwa ukiathiri sana jamii.
Hiyo ni kwa mujibu wa Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele----Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Bi Sheila Mbike
Alisema vimelea vya ugonjwa wa usubi huchelewa kujitokeza na kwamba inaweza kuchukua miaka mitano hadi 10.
"Ni vizuri kuchukua tahadhari kwani athari za ugonjwa huu ni kubwa---inaweza kupelekea upofu na hivyo kupunguza nguvu kazi," alisema Bi Sheila.
Kinga tiba ya usubi ni zoezi la kitaifa ambalo hufanyika kila mwaka chini ya Wizara ya Afya katika baadhi ya maeneo yenye maambukizi makubwa.
Kwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, zoezi hilo lilizunduliwa katika Kata ya Mbinga mjini B na Diwani wa kata hiyo Mh Sultan Andoya Alhamisi ya Agosti 17, 2023.
Ugonjwa wa usubi umekua pasua kichwa kwa muda mrefu si kwa Tanzania tuu, bali duniani kwote.
Mnamo Desemba 2015, zaidi ya wajumbe 200 kutoka mataifa 23 barani Afrika pamoja na mashirika ya kimataifa walikutana jijini Kampala, Uganda kujadili mikakati ya kutokomeza ugonjwa wa usubi.
Mpaka kipindi hicho (2015), ugonjwa huo uliathiri watu milioni 120 katika mataifa 35 duniani.
Katika kipindi hicho, barani Afrika pekee angalau watu 800,000 kati ya milioni 31 walioathirika walipoteza uwezo wa kuona.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.