Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, mkoani Ruvuma Mheshimiwa Vita Kawawa, amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Shilingi bilioni 7.798 kuboresha huduma ya majisafi na salama katika Mji wa Namtumbo.
Kawawa amesema hayo wakati anazungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wilayani Namtumbo katika ziara ya Katibu Mkuu CCM Balozi Dkt Emanuel Nchimbi akieleza kuwa hatua hiyo imeleta afueni kubwa kwa wananchi.
Katika hotuba yake, Kawawa amepongeza pia uamuzi wa Serikali kuruhusu kuendelea kwa utafiti wa mradi wa madini ya Uran, akifafanua kuwa mradi huo utakapotekelezwa utakuwa chanzo cha mapato kwa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
“Ndani ya kipindi cha miaka minne, Wilaya ya Namtumbo imepokea fedha zilizowezesha ujenzi wa shule tano za sekondari, ikiwemo Shule ya Sekondari Dkt Samia Suluhu Hassan iliyogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 4, na shule za Msisima na Hanga zilizogharimu Shilingi milioni 600 kila moja”,alisema Kawawa
Aidha, Kawawa amesema Serikali ya awamu ya sita imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 6.147 kujenga zahanati mpya 15, vituo vya afya, pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hatua ambayo imesaidia kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto wilayani humo.
Mbunge huyo amemuomba Katibu Mkuu wa CCM Taifa kuikumbusha Serikali kuhusu ahadi ya ujenzi wa barabara za Mtwarapachani–Nalas–Tunduru Mjini na Lumecha–Hanga–Malinyi hadi Ifakara kwa kiwango cha lami, akisisitiza kuwa barabara hizo ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Kawawa, ujenzi wa barabara hizo utachochea uchumi kwa kuwa maeneo yanayopitiwa yanazalisha mazao mengi ya chakula na biashara ambayo yanahitaji masoko ya uhakika na usafirishaji wa uhakika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Emanuel Nchimbi, amewataka Wakala wa Mbegu ASA kuongeza uzalishaji wa mbegu na kufungua ofisi wilayani Namtumbo ili wakulima wanufaike na juhudi za Serikali katika sekta ya kilimo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.