CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Mbinga na Nyasa (MBIFACU) katika msimu wa mwaka 2020/2021 kinatarajia kuongeza hekari 20 za miche ya kahawa ya kisasa(Compact) na kufikisha jumla ya hekari 71 za kahawa katika shamba la Ugano Mbinga .
Kaimu Meneja wa wa MBIFACU Henrick Ndimbo amesema upanuzi wa shamba la kahawa Ugano umelenga kuimarisha vitega uchumi wa MBIFACU na kuongeza mapato ya chama hicho ili kuweze kujitegemea na kuimarisha ushirika.
Ndimbo amesema miche ya kisasa ya kahawa katika hekari hizo 20 ipo 23,275 imepandwa msimu huu na kwamba mwaka 2023 MBIFACU inatarajia kuzalisha kahawa tani zaidi ya 23,000 ambazo zitawaingizia sh.milioni 69 ambazo zitaongeza mapato ya ndani ya chama.
Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa MBIFACU Winfred Lupembe amesema shamba hilo la kisasa la kahawa litaimairisha uchumi wa chama hicho na hatimaye MBIFACU itajitegemea kwa kila kitu kutokana na rasilimali zake.
Amesema katika shamba jipya miche ya kahawa imefunikwa kwa majani ili kuilinda miche hiyo wakati wa baridi na wakati wa jua kali isipate mwanga mkali na kuathiri miche kuwa na rangi ya njano ambayo inapoteza ubora wa kahawa.
‘’Shughuli zote ambazo tunazifanya MBIFACU zinalenga kuongeza ajira kwa vijana katika Wilaya ya Mbinga,lakini jambo kubwa zaidi ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kwa kauli yake ya kuimarisha ushirika nchini’’,alisisitiza Lupembe.
Akizungumzia historia ya shamba hilo Kaimu Meneja wa MBIFACU Henerick Ndimbo anasema katika kijiji cha Ugano, wanamiliki eneo la hekari 1052 na kwamba bado wana shamba la zamani la kahawa lenye ukubwa wa hekari 50 ambalo lina miche ya kahawa yenye umri wa zaidi ya miaka 100,
Hata hivyo amesema walipokabidhiwa miche hiyo kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha MBICU,waliamua kuifufua upya miche hiyo na kuacha baadhi ya miche ya zamani inayotumika kama shamba darasa.
“Hii miche ya zamani ya kahawa ukiitunza vizuri inaweza kutoa hadi kilo tano kwa mche mmoja,msimu uliopita tuliweza kupata hadi tani 2.6 za kahawa kwa miche ya zamani ambazo zilituingizia milioni tisa.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa MBIFACU Winfred Lupembe amesema katika kuliboresha shamba la zamani la kahawa chama hicho kina mpango wa kufuga ng’ombe ambao watawawezesha kupata mbolea ya samadi ambayo itatumika kuweka kwenye kahawa.
Lupembe amesisitiza kuwa shamba hilo baada ya muda sio mrefu litabadilika na kustawi hali ambayo itaongeza uzalishaji wa kahawa na kwamba MBIFACU katika shamba hilo pia inatarajia kupanda migomba ambayo itakuwa zao la biashara katika kuongeza mapato kwa Chama hicho.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Ruvuma Bumi Masuba anatoa rai kwa Vyama vya ushirika nchini kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ili viwe na vyanzo vingine vya mapato badala ya kutegemea ushuru wa mazao ya mkulima.
“Msimu uliopita Chama Kikuu cha Ushirika MBIFACU kilikuwa kinatoza ushuru shilingi 40 kwa kilo,kutokana na uboreshaji wa miradi ya chama,ushuru umeshushwa kuanzia Julai mosi 2020,mkulima anatozwa sh. 30 kwa kilo na tutaendelea kushusha kadri miradi ya uwekezaji itakavyoimarika’’,alisisitiza.
Amesema miradi kwa vyama vya ushirika pia ina muongezea mkulima mapato kwa kuwa na gawio la faida kwa sababu kadiri vyama vinavyoongeza mapato ndiyo inavyotengenezwa faida kwa mkulima.
MBIFACU inamiliki shamba lenye ukubwa wa hekari 1052 katika eneo la Ugano,ambapo baadhi ya maeneo wameweka wawekezaji wanaoendeleza likiwemo shamba la kahawa ya TACRI Ugano.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 8,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.