WAKALA wa barabara za vijijini na mijini(Tarura) wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,umeishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuipatia jumla ya Sh.milioni 495,000,000 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 zilizotumika kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Meneja wa Tarura wilaya ya Namtumbo Mhandisi Fabian Lugalaba, wakati akizungumza kuhusiana na barabara mpya zilizojengwa na Tarura ambazo zimewezesha kuunganisha vijiji mbalimbali na kuchochea uchumi wa wananchi.
Lugalaba alisema, kati ya fedha hizo Sh.milioni 90,000,000 zimetumika kwa ajili ya kujenga(kutoboa) barabara mpya na kiasi cha Sh.milioni 405,000,000 zimetumika kujenga madaraja yaliyowezesha kurudisha mawasiliano kwa vijiji vya Mgombasi,Miembeni na Likuyumandela.
Kwa mujibu wake,katikati ya kata ya Mgombasi na Likuyuseka kuna kijiji cha Miembeni ambacho hakikuwa na mawasiliano ya barabara,hivyo kusababisha wakazi wake kuwa na mazingira magumu pindi wanapohitaji kwenda maeneo mengine kwa ajili ya kupata huduma ikiwamo ya afya.
Alisema,kutokana na changamoto hiyo serikali iliona umuhimu wa kupeleka barabara katika maeneo hayo ambapo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ilitenga jumla ya Sh.milioni 90 kwa ajili ya kutoboa(kujenga)barabara mpya itakayounganisha kata hizo na kijiji hicho.
Lugalala alitaja barabara hizo ni Mfuate-Miembeni-Mgombasi yenye urefu wa km 17.2 iliyogharimu juma ya Sh.milioni 50 na barabara ya Likuyumandela-Miembeni yenye urefu km 11.5 iliyojengwa kwa gharama ya Sh.milioni 40.
Aidha alisema,katika maeneo hayo yote mawili kuna mito ambayo ilihitaji kujengwa madaraja,ambapo katika barabara ya Mfuate-Miembeni- Mgombasi kulihitaji daraja la mita 20 katika mto Luegu na limejengwa kwa gharama ya Sh.milioni 350.
Lugalaba alitaja daraja lingine ni la mita 8 linalounganisha kijiji cha Miembeni kwenda Likuyumandela ambalo hadi kukamilika limegharimu sh.milioni 40.
Alieleza kuwa,kwa kutumia fedha zinazoletwa na Serikali zikiwamo za ongezeko la tozo zilizoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, watahakikisha wanajenga miradi ya barabara kwa ubora wa hali ya juu,uaminifu,uadilifu na inayoendana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa ili wananchi wengi hasa waishio maeneo ya vijijini wafikiwe na mtandao wa barabara.
Alisema,malengo ya Tarura ni kuhakikisha maeneo yote ambayo hayafikiki kwa urahisi wanatumia fedha zinazotengwa na Serikali kufikisha huduma ya mawasiliano ya barabara ili kuwarahisishia wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo.
Amewaomba wananchi ambao barabara na madaraja yamejengwa,kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo na kila mmoja kuwa mlinzi kwa mwenzake ili iweze kudumu na kwa muda mrefu.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Likuyumandela,Mfuate na Miembeni, wameishukuru serikali kwa jitihada za kurudisha mawasiliano ya barabara katika maeneo hayo.
Ali Mtima mkazi wa kijiji cha Miembeni alisema,kabla ya kujengwa kwa daraja katika mto Luegu linalounganisha kijiji hicho na Mgombasi,walilazimika kupita kwa shida katika mto huo wenye maji mengi hasa kipindi cha masika.
Mtima alisema,baadhi ya watu wamepoteza maisha kwa kusombwa na maji pindi wanapohitaji kwenda kijiji jirani cha Mgombasi kufuata huduma mbalimbali za kijamii ikiwamo huduma za afya.
Issa Amir mkazi wa Mgombasi, ameishukuru Tarura kwa kujenga barabara zinazounganisha kata ya Mgombasi na Likuyu kwani zimerahisisha mawasiliano na kuchochea kukua kwa uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
Alisema baada ya kujengwa kwa barabara hizo, sasa wanasafirisha mazao kutoka mashambani kwenda sokoni kwa urahisi na wafanyabiashara wengi wanafika kwa ajili ya kununua mazao wanayozalisha.
MWISHO.
6 Attachments • Scanned by Gmail
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.