MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua wiki maalum ya upandaji miti katika Mkoa wa Ruvuma ambapo jumla ya miti ya asili 3500 imepandwa.
Uzinduzi wa zoezi hilo umefanyika katika vyanzo viwili ambavyo ni chanzo cha Mto Luegu kilichopo katika Kijiji cha Ngwinde Kata ya Litola Wilaya ya Namtumbo na chanzo cha Mto Mgugusi kilichopo hifadhi ya Lugumbilo Kata ya Mbingamhalule Wilaya ya Songea.
Katika chanzo cha mto Luegu jumla ya miche ya miti ya asili 1500 imepandwa na katika chanzo cha Mto Mgugusi jumla ya miti ya asili 2000 imepandwa kwenye chanzo hicho. Miche ya miti hiyo imetolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu amesema wilaya hiyo inatekeleza maagizo ya kuhifadhi vyanzo vya maji kama yalivyotolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo kwa kuanzia amesema wameamua kupanda miti kwenye chanzo cha Mto Luegu na kuendelea kwenye mito yote inayoingiza maji kwenye mto huo.
Akizungumza baada ya kuzindua upandaji miti kwenye chanzo cha Mto Luegu,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekitaja chanzo hicho kuwa kina umuhimu mkubwa kitaifa kwa sababu Mto Luegu unachangia maji asilimia 19 katika Mto Rufiji.
“Mto huu Luegu ambao tumekuja leo kupanda miti kwenye chanzo chake unachangia asilimia 19 ya maji yote yanayokwenda kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere kupitia Mto Rufiji,tunatarajia mradi huu ukikamilika unakwenda kumaliza tatizo la upungufu wa nishati ya umeme nchini’’,alisisitiza RC Thomas.
Amesema kutokana na umuhimu wa chanzo hicho amepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu kwenye chanzo cha Mto huo ili kiwe endelevu.
Hata hivyo amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Ngwinde kwa kulinda hifadhi ya msitu huo wenye chanzo hicho ambapo ametoa rai kwa TFS kuwagawia bure wananchi hao miche ya asili nay a matunda ili waweze kupanda na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza baada ya kuzindua upandaji miti chanzo cha Mto Mgugusi unaomwaga maji yake katika Mto Ruvuma,Mkuu wa Mkoa amesikitishwa na uharibufu mkubwa wa hifadhi ya msitu wa Lugumbilo uliopo kwenye chanzo hicho ambapo wananchi wamelima na kuharibu chanzo hicho.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea kuhakikisha watu wote waliohusika na uharibifu wa chanzo hicho wakamatwe na kufunguliwa mashtaka kwa sheria ya kuharibu hifadhi ya mazingira na kwamba wote waliolima mashamba ya mahindi kwenye chanzo hicho waondolewe na hifadhi ibaki wazi.
Ameagiza milima yote ya hifadhi katika Mkoa wa Ruvuma ambayo imevamia na wananchi wakifanya shughuli za kibidamu wote waondolewe ili kulinda vyanzo vya maji kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Komred Odo Mwisho akizungumza baada ya kupanda miti kwenye vyanzo hivyo amekemea uharibufu wa mazingira kwenye chanzo cha Mbingamhalule na ameunga mkono hatua za serikali kuwachukulia hatua wote wanaoharibu mazingira.
Naye Mshauri wa Maliasili Mkoa wa Ruvuma Africanus Challe amesema katika wiki maalum ya upandaji miti inayoanzia Januari Mosi hadi 7,2023 katika Mkoa wa Ruvuma inatarajiwa kupandwa miche ya miti ya asili 1,100,000 iliyotolewa na TFS .
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.