Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia Idara ya Mipango mji kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Aga Teo Hope Foundation wanatekeleza mradi wa urasimishaji wa viwanja 5260 katika mji mzima wa Peramiho.
Afisa Mipango Miji wa Halmashauri hiyo Meliladius Aliefao anasema zoezi hilo limelenga kurasimisha mji mzima wa Peramiho ambapo anasema Taasisi ya Aga Teo Hope Foundation imeletwa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha kila kipande cha ardhi katika mji wa Peramiho na Halmashauri ya Wilaya hiyo vinapimwa.
“Mkoa wa Ruvuma umewekewa lengo la kurasimisha kwa mwaka watu 7000,sisi kama Halmashauri tumejiwekea ndani ya miezi mitatu kutoka sasa kurasimisha viwanja wananchi zaidi ya 5000’’,anasema Aliefao.
Anasema hadi kufikia Desemba mwaka huu watu zaidi ya 5000 watakuwa wamerasimishwa viwanja vyao kwa kupimiwa, kupangiwa na kumilikishwa na kwamba katika zoezi hilo wananchi wanachangia gharama kulingana na mkubaliano baina ya Halmashauri,Taasisi ya AgaTeo na wananchi wenyewe.
Afisa Mipango Miji huyo anasema wananchi wamekubali kuchangia kiasi cha shilingi 150,000 ambayo hawatalazimika kuichangia kwa mara moja kwa sababu Taasisi ya Aga Teo imefadhili sehemu kubwa ya gharama zinazohitajika kutekeleza mradi huo.
Anasema hadi sasa tayari wananchi wameunda Kamati zao na kufungua akaunti zao ambazo wataweka michango yao taratibu na kwamba wananchi watalazimika kukamilisha michango yao hadi hapo Halmashauri itakapokamilisha hati zao.
Kwa upande wake William Mapunda ambaye ni Mratibu wa Taasisi ya Aga Teo Hope Foundation anasema wanatekeleza mradi wa urasimishaji wa viwanja katika Halmashauri ya Songea na kwamba Taasisi hiyo ilisajiriwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2019 kupitia TAMISEMI na kazi kubwa ya Taasisi hiyo ni kurasimisha ardhi na mashamba katika miji na vijiji.
Mapunda anasisitiza kuwa wamedhamiria kuhakikisha kuwa wananchi wanapata hatimilki ambazo zitawezesha kukopesheka na Taasisi za kifedha kwa upande wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu.
Anazitaja kata sita ambazo wanaanza kutekeleza mradi wa urasimishaji ardhi kuwa ni Kata ya Peramiho,Liganga, Kilagano, Litisha,Parangu na Mbingamhalule.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Septemba 14,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.