Mkoa wa Ruvuma umeshika nafasi ya kumi kitaifa kati ya mikoa 26 nchini kwenye mashindano ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2023.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Ruvuma Zuberi Mshamu wakati anatoa taarifa ya tathimini ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kwenye maandalizi ya Mbio za mwenge wa Uhuru 2024 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Mshamu amebainisha kuwa katika mashindano ya Mwenge wa Uhuru kitaifa 2023 Mkoa wa Ruvuma ulipata alama 76.27 na kushika nafasi ya kumi ambapo kimkoa Halmashauri ya Mbinga mji iliyoongoza kwa alama 82.98 na kwamba Halmashauri hiyo imeshika nafasi ya 14 kitaifa.
Kulingana na Mratibu huyo Halmashauri ya Manispaa ya Songea kimkoa imeshika nafasi ya pili kwa alama 80.06 ambapo kitaifa imeshika nafasi ya 37,Halmashauri ya Tunduru ya tatu ikiwa na alama 77.96,kitaifa ikiwa imeshika nafasi ya 53 na Halmashauri ya Namtumbo imeshika nafasi ya nne kimkoa ikiwa na alama 77.82 na kitaifa ikiwa imeshika nafasi ya 55.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo,Halmashauri ya Madaba kimkoa imeshika nafasi ya tano ikiwa na alama 74.93,kitaifa imeshika nafasi ya 107,Halmashauri ya Mbinga kimkoa imeshika nafasi ya sita ikiwa na alama 73.57 ambapo kitaifa imeshika nafasi ya 130,Halmashauri ya Songea kimkoa imeshika nafasi ya saba ikiwa na alama71.86 ambapo kitaifa imeshika nafasi ya 152 na Halmashauri ya Nyasa kimkoa ya nane ikiwa na alama 71 na kitaifa ya 159.
“Timu ya uratibu ya Mkoa inatoa pongezi kwa uongozi wa Wilaya zote na wananchi kwa ujumla kwa kazi kubwa ya kufanikisha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2023 na mwaka huu tuongeze bidii Zaidi kuhakikisha mwaka 2024 tufanya vizuri zaidi’’,alisisitiza Mshamu.
Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza kwenye kikao cha maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2024 mkoani Ruvuma ameagiza kuhakikisha miradi itakayochaguliwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru inakuwa na ubora na kukidhi vigezo vyote.
Amesisitiza mambo ya msingi na vigezo vyote vilivyowekwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu kuzingatiwa na kufanyiwa kazi ikiwemo uhifadhi wa mazingira na uendelevu wa upandaji miti katika wilaya zote mkoani Ruvuma.
“Mwenge ni nembo ya ishara inayomwakilishi Mheshimiwa Rais kwa hiyo inatakiwa kujitoa kikamilifu jambo ambalo ni heshima yetu ya utii kwake hata kama hayupo chombo kile kinamwakilisha yeye’’,alisistiza Kanali Abbas.
Mwenge wa Uhuru unatarajia kuanza mbio zake mkoani Ruvuma Juni 8,2024 na kukamilisha mbio zake Juni 16,2024 ambao utakimbizwa katika Wilaya tano na Halmashauri nane.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.