WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema baada ya serikali kuboresha uwanja wa ndege wa Songea baadhi ya wananchi wa Malawi na Msumbiji wanatumia kiwanja hicho kupanda ndege Kwenda Dar es salaam.
Mheshimiwa Majaliwa ameeleza hayo wakati anazungumza kwenye kilele cha Jubilei ya miaka 125 ya uinjlishaji wa kanisa katoliki Jimbo Kuu la Songea iliyofanyika Abasia ya Peramiho nje kidogo ya mji wa Songea ambapo Waziri Mkuu alikuwa ni mgeni rasmi.
“ Baba Askofu Mkoa wa Ruvuma hivi sasa una fursa nyingi ambazo kanisa pia mnaweza kuzitumia,serikali imeboresha na kuimarisha uwanja wa ndege wa Songea,taa za kuwezesha ndege kutua mchana na usiku zimewekwa na baada ya kuanzisha safari za ndege mara tatu kwa wiki tumegundua kuwa watu wa Msumbiji na Malawi wanafika hapa kupanda ndege na Kwenda Dar es salaam’’,alisisitiza Waziri Mkuu.
Amesema mji wa Songea hivi sasa umetengeneza mzunguko hadi nchi jirani hivyo serikali inalazimika kuongeza safari za ndege kutoka mara tatu hadi walau mara tano kwa wiki hivyo ametoa rai kwa Mkurugenzi wa ATCL kuona uwezekano wa kuongeza ndege kwa kuwa zilizopo zinajaa na hazitoshi kwa mahitaji ya wananchi.
Akizungumza kwenye Jubilei hiyo Waziri Mkuu amezitaja fursa nyingine za kiuchumi zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma ambazo madhehebu ya dini yanaweza kuzitumia kuwa ni sekta ya kilimo ambapo amesema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa mitano bora inayoongoza kwa kuzalisha mazao chakula nchini.
Amesema serikali inaendelea na mikakati yake ya kufungua fursa za kibiashara kwenye Mkoa wa Ruvuma ambapo tayari umeme wa gridi umeunganishwa mkoani Ruvuma na kwamba Mkoa umeunganishwa kwa barabara za lami katika wilaya zote na sasa kazi ya kuunganisha barabara za lami ndani ya wilaya inaendelea.
Fursa nyingine amezitaja kuwa ni fursa ya madini,misitu,utalii na uvuvi ambapo ametoa rai kwa madhehebu ya dini kuangalia fursa zilizopo katika maeneo hayo na kwamba serikali ipo tayari kutoa leseni ili madhebeu ya dini yaanze mara moja kutumia fursa hizo.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na viongozi wa dini ambapo amempongeza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea Mhashamu Damian Dallu kwa kuadhimisha jubilei ya miaka 125.
Amesema katika kipindi chote hicho kanisa limefanikiwa kuwajenga waumini wake kiimani na kuwaelimisha namna waumini wanavyoweza kukuza uchumi wa mtu binafsi.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho kanisa limekuwa mstari wa mbele kuunga mkono kwa vitendo jitihada za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo kwa kujenga shule,vituo vya afya,viwanda,vituo vya kulelea Watoto yatima,kuanzisha vyuo mbalimbali vya ufundi stadi na kuanzisha vyuo vikuu ambapo amesisitiza kuwa kazi hiyo imeleta maendeleo makubwa katika ustawi wa jamii.
Awali akizungumza kabla ya Waziri Mkuu kuzungumza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea Mhashamu Damian Dallu amesema kanisa linaadhimisha jubilei ya uinjilishaji iliyoletwa na wamisionari wabenediktini mwaka 1898 likiwa limepata mafanikio makubwa kimwili na kiroho kutokana na wamisionari wabenediktini kupanda mbegu ya injili iliyozaa matunda kwa kipindi cha miaka 125.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye jubilei hiyo amesema Serikali kwa kushirikiana na kanisa wameweza kuleta mafanikio makubwa kwa wananchi katika sekta za elimu,afya,barabara na miundombinu na kwamba serikali ya Mkoa ipo tayari kuendelea kushirikiana na viongozi wa dini ili kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema Jubilei hiyo imeweka historia nyingine kwa kutimiza miaka 125 ya uinjilishaji ambao ulianzia Peramiho mwaka 1898.
Amebainisha kuwa jubilei ya miaka 125 inakwenda kufungua aina mpya ya utalii wa hija hivyo mji wa Peramiho unatarajia kuanza kupokea wageni wengi wa kitaifa na kimataifa ambayo watakuwa wanafika kufanya utalii wa hija.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.