MKOA wa Ruvuma una ziada ya chakula tani 787,190 hali iliyosababisha Mkoa kuendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika uzalishaji mazao ya chakula.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anafungua kikao cha Baraza Ushauri la Mkoa (RCC) kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Amesema katika msimu wa mwaka 2021/2022 Mkoa uliweza kuvuna mazao ya chakula tani 1,256,362 ambapo mahitaji ya chakula katika Mkoa ni tani 469,172 hivyo Mkoa kuwa na ziada.
Akizungumzia Mfumo wa mbolea ya ruzuku Kanali Thomas amesema Mkoa umeweza kusajili wakulima 261,235 kati yao wakulima 250,493 wameshaingizwa kwenye Mfumo na kupata mbolea ya ruzuku. “Tunaishukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha Mfumo wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima kwani hivi sasa wakulima wanapata mbolea kwa bei karibia na nusu ya bei ya mbolea ya msimu uliopita “,alisema Kanali Thomas.
Kuhusu Mfumo wa stakabadhi ghalani RC Thomas amesema Mkoa unaendelea kusimamia Mfumo huo kutokana na mafanikio makubwa kwa wakulima.
Amesema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 katika zao la ufuta pekee kupitia stakabadhi ghalani wakulima wamepata zaidi ya shilingi bilioni 23 baada ya kuuza kilo 7,970,176.
Amesema pia wakulima katika msimu huo wameingiza zaidi ya shilingi bilioni 11 baada ya kuuza soya na mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Desemba 28,2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.