Serikali imejumuisha utoaji wa huduma za chakula na lishe shuleni kama kiashiria kwenye mkataba wa lishe unaotekelezwa katika mikoa yote Tanzania Bara.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya lishe Mkoa wa Ruvuma ambayo yamefanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya Songea Girls, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema ukosefu wa lishe unaathiri ustawi wa kimwili, utendaji wa kiakili kwa vijana na kuhatarisha uwezo wao katika taaluma hususani ufaulu wa mitihani shuleni.
Amesema Vijana balehe wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe ikiwemo utapiamlo wa aina mbalimbali hususani uzito pungufu , upungufu wa vitamini , madini na uzito uliopitiliza pia watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 9 na vijana balehe wenye umri wa miaka 10 hadi 19 wanakabiliwa na upungufu wa damu asilimia 42.
Amelitaja lengo la maadhimisho haya ni maalumu kwa ajili ya kusherehekea mafanikio, kuimarisha juhudi zinazoendelea kufanyika na kuongeza uelewa kwa umma kuhusu faida za lishe bora na madhara ya utapiamlo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Kampeni ya lishe kwa vijana balehe inalenga kuhamasisha sekta na wadau mbalimbali wa masuala ya lishe nchini kuweka kipaumbele katika masuala ya lishe kutenga bajeti ya utekelezaji wa shughuli za lisha ya vijana balehe, ili kuongeza uelewa katika jamii kuhusu uhusiano uliopo kati ya lishe bora na ustawi wa maisha ya vijana balehe sasa na baadae”, amesema Thomas.
Hata hivyo amesema ulimwenguni kote kuna vuguvugu kubwa la kutambua vijana kama kundi muhimu katika jamii ambapo wanakadiriwa vijana kuwa bilioni 1.2 wenye umri wa miaka 10 hadi 19.
Ameongeza kuwa idadi ya vijana inaongezeka kwa kasi na inatarajiwa kuongezeka mara dufu ifikapo mwaka 2050. Kusini mwa jangwa la sahara idadi ya vijana balehe inakadiriwa ni asilimia 23 ya watu wote na nchini Tanzania, vijana balehe wakadiriwa kuwa ni takribani robo ya watu wote kwa ujumla.
Imeandikwa na Farida Baruti
Kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.