MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameiagiza kampuni ya uchimbaji makaa ya mawe ya Market Insight Limited kuanza kazi mara moja ya uchimbaji katika kata ya Ruanda wilayani Mbinga.
Kampuni hiyo ilisimamisha kazi ya uchimbaji tangu Desemba 2019 kutokana na mgogoro baina ya wabia wa uchimbaji wa madini hayo hali iliyosababisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuunda Tume ya uchunguzi wa mgogoro huo iliyofanyakazi kwa siku 14.
Akitoa maagizo hayo kwa wadau wa madini mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake mjini Songea Mndeme ameuagiza uongozi wa Kampuni hiyo kuanza uzalishaji wa makaa ya mawe kuanzia Septemba 4,2020 na kuhakikisha wanalipa madeni yote wanayodaiwa na serikali.
“Mnadaiwa mrabaha wa zaidi ya shilingi milioni 274,deni hili lilipwe mara moja kuanzia leo, na deni la kodi ya huduma mnalodaiwa na Halmashauri lilipwe mara moja’’,amesisitiza.
Mndeme pia ameagiza madeni mengine ya kodi ambayo Kampuni hiyo inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA yalipwe kuanzia sasa na ameagiza Mhandisi wa Madini wa Kampuni ya Market Insight Limited Fredrick Mwaipopo ambaye anatuhumiwa kukimbia na shilingi milioni 62 za mishahara ya watumishi wa mgodi atafutwe ili kujibu tuhuma hizo.
Mkuu wa Mkoa ameiagiza kampuni hiyo kuanza kuuza makaa ya mawe kwenye viwanda vya ndani ili kupata nishati ya kutosha na ziada inayobaki isafirishwe kwenda nje ya nchi.
Mndeme pia ameagiza Kampuni hiyo kutoa ajira kwa Watanzania, kuchimba makaa ya mawe yenye viwango ili soko lipanuke, na kuzingatia afya za watumishi wote wanaofanya kazi katika mgodi huo na usalama wa mazingira ya mgodi huo.
Mkuu wa Mkoa amewaasa wasimamizi wa mgodi huo kutokuwa na migogoro na kwamba wanapotofautiana wamalizane wao kwa kwao chini ya usimamizi wa Afisa madini wa Mkoa .
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye ameutaka uongozi wa kampuni hiyo kutekeleza maagizo yote ya serikali yaliyotolewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, ikiwemo kupima afya ya watumishi wanaofanya kazi katika mgodi huo,kuwapatia vifaa vya usalama kazini vikiwemo Barakoa na buti.
Naye Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Mohamed Nkana ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambapo ameitaka Kampuni ya Marketi Isight Limited kutekeleza maagizo hayo na kwamba wakiendelea na migogoro watachukuliwa hatua ikiwemo kunyang’nywa leseni za uchimbaji wa madini.
Imeandaliwa na Aneth Ndonde na Farida Mussa
Ofisi ya Habari ya Mkoa wa Ruvuma
Septemba 4, 2020.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.