MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme Aprili 24,2020 amefungua rasmi minada ya mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani katika Mkoa wa Ruvuma kwa msimu wa mwaka 2019/2020.
Ufunguzi huo umefanyika ofisini kwake mjini Songea mbele ya wanahabari wachache bila kuwa mkusanyiko wa watu ili kukabiliana na maambukizi ya virusi hatari vya corona.
Mndeme akizungumza kwenye uzunduzi huo ameyataja mafanikio yaliyopatikana katika msimu uliopita wa 2018/2019 kuwa ni kuongezeka kwa pato la mkulima kutokana na mauzo mazuri.
Amesema katika msimu huo katika zao la ufuta ziliuzwa kilo 8,428,268 kwa wastani wa bei ya shilingi 2,959 kwa kilo ambazo ziliwawezesha wakulima kupata zaidi ya shilingi bilioni 24.
“Katika kipindi hicho zao la soya zilizopatikana ni kilo 2,858,383 ambazo ziliuzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 750 na kuwawezesha wakulima kupata kiasi cha shilingi bilioni 2,143,787,250.00 kupitia minada ya Namtumbo na Songea’’,alisema.
Hata hivyo Mndeme amesema katika kipindi hicho zao la mbaazi zilipatikana kilo 773,543 ambazo ziliuzwa kwa wastani wa shilingi 700 kwa kilo na kuwawezesha wakulima kupata zaidi ya shilingi milioni 541.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,matarajio ya msimu huu ni kukusanya na kuuza ufuta na soya zaidi ya tani 12,108 na mbaazi tani 17,711 na kwamba minada hiyo itafanyika katika vituo vitatu ambavyo ni Songea,Namtumbo na Tunduru.
Hata hivyo amesema mnada huo utakuwa na watu wachache wanaowakilisha wakulima na wanunuzi ili kuondoa mikusanyiko kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa korona kama inavyoshauriwa na watalaam wa afya.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 24,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.