MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amegawa vitambulisho 9000 vya wajasiriamali wadogo kwa wakuu wa wilaya zote ili waende kuvigawa kwa walengwa.
Mndeme amegawa vitambulisho hivyo katika hafla fupi iliyofanyika nje ya viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea na kushirikisha wakuu wa Wilaya zote,Makatibu tawala ,Maafisa Tehama,Maafisa Biaashara na Meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza kabla ya kugawa vitambulisho hivyo Mdeme amesema Rais Dkt John Magufuli ametoa vitambulisho hivyo ambapo mwaka huu, Mkoa wa Ruvuma umepangiwa jumla ya vitambulisho 58,000 na kwamba katika awamu ya kwanza vimeletwa vitambulisho 9000 na kwamba katika awamu ya pili Mkoa utaletewa vitambulisho 49,000.
Amesema Vitambulisho vitatolewa kwa wajasiriamali wadogo wenye sifa waliopo katika kila Halmashauri ambapo utaratibu wa ugawaji kwa mwaka huu ni wa kutumia mfumo wa kompyuta ili kuwawezesha kutunza kumbukumbu ya wafanyabiashara na watoa huduma.
“Nawaelekeza maafisa Biashara kuhakikisha fomu ya maombi ya kitambulisho inajazwa na pesa inayokusanywa iwekwe Benki ,kila risiti moja ya malipo ya shilingi 20,000 itatumika kusajiri mfanyabiashara mmoja’’,amesisitiza.
Ameutaja mchanganuo wa mgao wa vitambulisho hivyo mwaka huu katika awamu ya kwanza kuwa Wilaya ya songea imepewa vitambulisho 3,500,Mbinga vitambulisho 2000,Tunduru vitambulisho 1500,Namtumbo vitambulisho 1000,na Nyasa imepata vitambulisho 1000.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa,Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Steven Ndaki amelitaja lengo la kuwagawa vitambulisho hivyo ni kuwarahisishia wafanyabiashara wadogo katika biashara ili waondokane na usumbufu hivyo kufanya kazi kwa ufanisi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema amesema mwaka jana Wilaya ya Songea Ilipewa Vitambulisho 15,000 ambavyo walifanikiwa kuvigawa vyote kwa wajasiriamali wadogo na kwamba mwaka huu wajasiriamali wadogo wanavisubiri vitambulisho hivyo kwa hamu kubwa.
Mwaka 2019,Rais Dkt John Magufuli aligawa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo 60,000 katika Mkoa wa Ruvuma ambapo hadi kufikia Mei 19, mwaka huu Mkoa ulifanikiwa kugawa vitambulisho 55,607 na kukusanya shilingi 1,112,135,000/=
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Mei 21,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.