Matatizo ya mimba za utotoni hapa nchini yamekuwa yanaongezeka mwaka hadi mwaka hali ambayo inaathiri wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) inaitaja mikoa inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha mimba za utotoni kuwa ni mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa asilimia 59,Tabora asilimia 58,Mara 55,Dodoma 51 na Lindi asilimia 48.
Mikoa mingine ni Mbeya asilimia 45,Singida asilimia 42,Rukwa asilimia 40,Ruvuma asilimia 39,Tanga asilimia,29,Arusha asilimia 27,Kilimanjaro asilimia 27, Kigoma asilimia 20,Dar es salaam asilimia 19 na Iringa asilimia nane.
Mkoa wa Dodoma umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba na ndoa za utotoni ambapo asilimia 51 ya wasichana wenye miaka kati ya miaka 20 hadi 22 wameolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 mkoani humo, ukilinganisha na asilimia 37 ya kitaifa kwa mujibu wa takwimu.
Kwa mujibu wa takwimu hizo kati ya watoto 100, watoto 51 wanaoolewa kabla ya kufikia miaka 18 katika mkoa wa Dodoma ambapo watoto wanaozaa wakiwa na umri mdogo ni asilimia 39.
Mkoa wa Dodoma umezindua kampeni ya kupambana na ndoa na mimba za utotoni ili kufikia malengo ya kumkomboa mtoto wa kike na kumuweka katika mazingira salama ya kumuwezesha kufikia ndoto zake badala ya kukatizwa na mimba za utotoni.
Mkakati unaotumiwa hivi sasa ni ule unaojulikana kama magauni manne ambayo ni mtoto wa kike kuwa ndani ya sare ya shule, gauni la pili ni la kuhitimu masomo,gauni la tatu ni la harusi na gauni la nne ni la kuvaa wakati wa ujauzito ambapo mtoto wa kike aatakuwa ametimiza ndoto zake.
Ukiacha Mkoa wa Dodoma,katika mwaka mmoja uliopita wa 2016/2017 Mkoa wa Tabora ulikuwa na jumla ya mimba za utotoni 800 hali iliyosababisha mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa mitatu nchini inayoongoza kwa mimba za utotoni.
Kukithiri kwa vitendo vya mimba za utotoni kumesababisha Rais Dk.John Magufuli kutoa agizo la wanafunzi wote katika shule za msingi na sekondari ambao watapata mimba hawataruhusiwa kuendelea na masomo.
Mimba za utotoni ni tatizo ambalo linasababisha watoto wa kike kukatishwa masomo yao kila mwaka na kusababisha umaskini mkubwa katika familia na Taifa kwa ujumla.
Kwa mfano katika Mkoa wa Ruvuma takwimu za mwaka 2013 zilionesha kuwa,kiasi cha watoto wa kike 155 walishindwa kumaliza masomo yao ya shule za msingi na sekondari kutokana na mimba.
Mwaka 2006 Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa katika ziara ya mkoa wa Ruvuma alipotembelea wilaya ya Tunduru alisikitishwa na idadi kubwa ya wanafunzi zaidi ya 400 waliokuwa wameacha shule wakati huo kutokana sababu za mimba na utoro.
Takwimu za mwaka 2008 katika mkoa wa Ruvuma zilionesha kuwa jumla ya wanafunzi 544 walipewa mimba kati ya hao wanafunzi zaidi ya 300 kutoka wilaya ya Tunduru pekee.
Mafunzo ya unyago na msondo yanayofanywa na kabila la wayao wilayani Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma yanatajwa kusababisha idadi kubwa ya wanafunzi wa kike katika shule za msingi na sekondari kukatishwa masomo kwa kupata mimba na kuolewa kila mwaka.
Utafiti ambao umefanywa katika shule za sekondari za Frankweston,Mgomba,Tunduru,Mataka,Namwinyu, Lukumbule na Nalasi wilayani Tunduru unaonesha kuwa karibu nusu ya wanafunzi wa kike katika shule hizo waliacha masomo yao baada ya kupata mimba na kuolewa.
Azizi Saidi mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Frankweston anasema utamaduni wa kufanyiwa unyago umesababisha wanafunzi wa kike kupata mafunzo hayo na kujiona kwamba wapo tayari kuolewa hata wakiwa bado shuleni hali ambayo inasababisha wanafunzi wengi wa kike kuacha masomo.
Hemed Ally mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya Frank Weston anasema wanafunzi wa kike baadhi ya mambo ambayo wanafundishwa hayalingani na umri wa wanafunzi kwa kuwa ni mambo ya ndoa yanayohusu namna ya kuishi na wanaume watu wazima.
Anasema katika mafunzo hayo wanafunzi wa kike wanaelezwa faida za kuishi na mume lakini hawafundishwi madhara ambayo wanaweza kupata kwa kushiriki katika ndoa wakiwa wadogo hali hiyo ndiyo inawahamasisha wanafunzi kujiingiza kwenye ngono na kushawishika kuolewa wakiwa wanafunzi.
Katika kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mtoto wa kike ambaye ameshavunja ungo anatolewa katika nyumba ya wazazi na kupewa chumba cha pekee yake na kwamba mtoto huyo anakuwa huru kufanya lolote na kurudi nyumbani majira yeyote bila kuulizwa na mlezi au mzazi wake.
Utafiti kuhusu mimba za utotoni kwa wasichana uliofanywa mwaka 2010 na Chama cha waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), zinatoa picha ya kutisha. Mfano, mkoani Tabora pekee wasichana wa shule 819 walipata mimba kipindi cha mwaka 2006-2009. Na huko Morogoro kati ya mwaka 2007-2009 wasichana wa shule 331 walipata mimba na kukatisha masomo yao.
Bado takwimu toka Kitabu cha takwimu za Elimu Tanzania (BEST 2005-2009) zinaonesha kuwa watoto wa kike walioacha shule kuanzia mwaka 2005-2009 kwa sababu ya mimba za utotoni walikuwa 16,991. Na katika shule za sekondari wasichana walioacha shule kutokana na mimba kwa mwaka 2009 pekee walikuwa 4965.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wasichana 8000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi na wanafunzi zadi ya 5000 wa shule za sekondari.
Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha kuwa, tangu mwaka 2004 hadi 2008, wanafunzi wa kike 28,600 wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu za utoro mimba, na vifo.
Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha watoto wenye umri kuanzia miaka sifuri hadi miaka 14 ni zaidi milioni 19 sawa na asilimia 43.9 ya Watanzania wote.
Taarifa za kuwepo watoto milioni mbili nchini kutohudhuria shuleni zinatia doa jitihada za Serikali katika utekelezaji wa mipango ya Elimu kwa Wote ili kufikia malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Ripoti ya elimu ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2011,watoto milioni 57 duniani kote hawakuwepo shuleni kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba na utoro ambapo idadi kubwa ya watoto hao wanaishi barani Afrika.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Mohamed Safieldin anasema tatizo la mimba za utotoni kwa wanafunzi sio tu linasababisha kushindwa kuendelea na masomo bali pia huongeza kasi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).
Rasimu ya pili ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2010 imekiri kuwepo mdondoko wa wasichana na wavulana katika mfumo wa elimu kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za ujauzito, ndoa za utotoni, ajira za watoto na utoro.
Sera na sheria zilizopo katika Wizara ya Elimu zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa vitendo ili kupunguza au kumaliza tatizo la mimba za utotoni zinazosababisha idadi kubwa ya watoto wa kike kukatishwa masomo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari serikalini,mawasiliano yake ni albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.