MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewaagiza wadau mbalimbali wa ushirika,kuhakikisha kuwa ushirika unastawi kwa manufaa ya wanachama na taifa kwa ujumla.
Mndeme ametoa agizo hilo wakati anafungua kikao cha tathmini ya mfumo wa masoko kupitia vyama vya ushirika kilichofanyika kwenye ukumbi wa Songea klabu na kushirikisha wadau kutoka wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma.
Kwa mujibu wa Mndeme,ushirika unalindwa na sera na sheria ya ushirika na kwamba wanachama wenyewe ndiyo wasimamizi wa shughuli za kila siku za ushirika ambapo ameagiza katika Mkoa mzima pawe na mpango kabambe wa kusimamia,kuimarisha na kuendeleza ushirika.
”Tusiwaruhusu wanaotaka kupindisha sheria ili waue mfumo wa ununuzi wa mazao ya ufuta,mbaazi na soya katika Mkoa wetu,tusiwaruhusu wezi na wabadhirifu kuwa viongozi wa vyama vya ushirika’’,alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Amesema msimu wa masoko ya mazao ya jamii ya mikunde,ufuta,soya na mbaazi kwa mwaka 2019/2020 unatarajia kuanza Mei mwaka huu,hivyo ameagiza vyama vya msingi viandae vitendea kazi na vituo vya makusanyo,visimamie na kuanza makusanyo toka kwa wakulima.
Akitoa taarifa ya mazao ya ufuta,soya na mbaazi ,Meneja Mkuu wa SONAMCU Juma Mwanga amesema katika msimu wa mwaka 2019/2020 minada ya ufuta ilikuwa 19 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 16,minada ya soya 10 yenye thamani ya zaidi ya bilioni mbili na minada ya mbaazi mine yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 471.
Hata hivyo licha ya mafanikio yaliopatikana amezitaja changamoto zilizojitokeza katika kipindi hicho kuwa ni kukosekana kwa vifaa vya kusafishia ufuta,bei elekezi ya chini ukilinganisha na bei ya soko na wanunuzi kuchelewa kutoa mzigo ghalani.
Kwa muda mrefu vyama vya ushirika katika Mkoa wa Ruvuma vimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla kwa sababu ushirika ni njia muhimu ya maendeleo kwa watu wa vipato vyote.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 4,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.