MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaonya watumishi wa umma kutokuwa sehemu ya kuhujumu miradi ya maendeleo.
Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea katika mji Mdogo wa Peramiho RC Thomas amesema serikali haitasita kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote anayekwenda kinyume na Utumishi wa Umma.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amemuagiza Afisa Utumishi katika Halmashauri hiyo kusimamia haki za watumishi ikiwemo kupandishwa vyeo kwa wakati.
Amesisitiza kujenga na kuimarisha mahusiano katika sehemu za kazi na kufanya kazi kwa kushirikiana baina ya wakuu wa Idara na watumishi wa chini.
“Watumishi jiepusheni na mikopo yenye riba kubwa,watumishi msiishi maisha fake yanasababisha kuingia kwenye madeni makubwa jambo ambalo ni hatari kwa mtumishi“,alisisitiza.
Katika hatua nyingine Kanali Thomas ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Songea kuanzisha mashamba ya pamoja (Block farming) na kusisitiza kuwa serikali inaendelea kuboresha Mfumo wa usambazaji mbolea ya ruzuku ili kuisogeza jirani na wakulima.
Mkuu wa Mkoa amepiga marufuku uingizaji Mifugo mkoani Ruvuma na kwamba zoezi la kuondoa Mifugo katika maeneo yasiyostahili linaendelea katika Mkoa mzima.
Mkuu wa Mkoa pia ameagiza kuongeza ukusanyaji mapato kwa kusimamia ipasavyo ukusanyaji kwa kutumia mashine za kukusanyia (POS)na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Neema Maghembe ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo Maghembe amesema ukusanyaji mapato katika Halmashauri hiyo unaridhisha ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri hiyo ilikusanya shilingi bilioni 1.7 sawa asilimia 115.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea ni miongoni mwa Halmashauri tatu zinazounda Wilaya ya Songea iliyoanzishwa mwaka 1984.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.