MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mheshimiwa Aziza Mangosongo,amezindua miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa elimu huku akikemea tabia ya baadhi ya walimu wa kiume kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi wao.
Mheshimiwa Mangosongo alisema,tabia hiyo imechangia kuporomoka kwa maadili kwani baadhi ya walimu wanatumia nafasi zao kuwarubuni wanafunzi na kufanya nao mapenzi,hivyo kusababisha wanafunzi kufanya vibaya katika masomo yao.
MHE.Mangosongo ametoa kauli hiyo,alipokuwa akizungunza na walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari na viongozi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga kwenye uzinduzi wa miongozo hiyo katika Halmashauri ya wilaya Mbinga.
“kuna mwalimu mmoja sitaki kutaja jina lake na shule anayofundisha, amempa mimba mwanafunzi wake aliyetakiwa kujiandaa na mitihani ya kidato cha nne mwaka huu,lakini jambo la kusikitisha hata walimu wenzake hawataki kumtaja”alisema Mangosongo.
Alisema,Halmashauri ya wilaya Mbinga hakuna sababu ya kutofanya vizuri katika suala la kitaaluma kutokana na kuwepo kwa mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ikilinganisha na Halmashauri nyingine katika mkoa wa Ruvuma.
Mangosongo alieleza kuwa,miongozo hiyo hususani wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu ya msingi ni mikakati ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji,usimamizi na ufuatiliaji na ushiriki wa wadau ili kufanikisha utekelezaji huo.
Hivyo,amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari kutumia miongozo ya usimamizi na uendeshaji iliyotolewa na serikali kufanya tathimini ya mara kwa mara ya hali ya elimu ili kurudisha heshima ya wilaya ya Mbinga kitaaluma.
Amewaagiza,kuanza kuwafuatilia na kuwaandikisha watoto wote wenye umri wa kuanza elimu ya awali na shule ya msingi ili waanze masomo ifikapo mwezi Januari 2023 na kusimamia watoto watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wawe wameripoti mara shule zitakapofunguliwa.
Amewahimiza walimu kuwa wabunifu, kujifunza ikiwamo kusoma vitabu mara kwa mara ili kupata maarifa na mbinu mpya zitakazowasaidia kufanya vizuri katika kazi zao za kila siku.
Miongozo iliyozinduliwa katika Halmashauri hiyo,ni mkakati wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu ya msingi,uteuzi wa viongozi wa elimu katika mamlaka za serikali za mitaa na changamoto katika uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Juma Haji alisema,wamejipanga kufanya vizuri katika sekta ya elimu ili watoto wote waliopo kwenye shule za msingi na sekondari wapate elimu bora na hatimaye waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Naye Afisa elimu sekondari wa Halmashauri hiyo Peter Ntalamka alisema, Halmashauri ya wilaya Mbinga ina shule za msingi 167 kati ya hizo shule za serikali ni 164, na shule binafsi 3 na kwa upande wa sekondari kuna shule 47 ambapo za serikali 31 na binafsi 16.
Alieleza kuwa, kwa shule za msingi kuna wanafunzi 67,078 na sekondari 14,652 na mahitaji ya walimu wa shule za msingi 1,936 waliopo 938 pungufu 998 na sekondari mahitaji ya walimu 716 waliopo 535 na pungufu walimu 181.
Aidha alisema, mwaka 2022 uandikishaji kwa wanafunzi wa shule za msingi ulivuka lengo kwa asilimia 133 kwa darasa la awali na asilimia 123 kwa darasa la kwanza.
Kwa mujibu wa Afisa elimu huyo,kwa shule za sekondari uandikishaji ulikuwa asilimia 94 kwa kidato cha kwanza, na asilimia 76 kwa kidato cha tano,hata hivyo juhudi za kuhakikisha wanafunzi wote wanaandikishwa.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.