MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameviagiza vyombo vya dola kuhakikisha kuwa wadaiwa wote 1664 wanaohusika na upotevu wa shilingi bilioni 1.377 fedha za SACCOS 26 mkoani Ruvuma wanasakwa na kukamatwa.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya vyama vya kuweka na kukopa katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Songea klub,Mndeme amesema aliunda Tume ya kuchunguza ubadhirifu wa fedha katika SACCOS za mkoa wa Ruvuma kufutia madai ya baadhi ya wanachama kuibiwa fedha zao.
Amesema katika uchunguzi uliofanywa katika SACCOS 26 umebaini kuwa kuna upotevu wa kiasi hicho cha fedha ambapo amesema wahusika ni lazima warejeshe fedha hizo.
Mndeme amemuagiza Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma kuwakamata mameneja,wahasibu na wenyeviti wa Bodi za SACCOS 26 zilizohusika na upotevu wa fedha za wanachama kiasi cha shilingi bilioni 1.377.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa pia ameagiza viongozi wa zamani wa SACCOS hizo wanaotuhumiwa na upotevu wa fedha wasakwe na kukamatwa na kwamba iwapo wamefariki,warithi watahusika na ulipaji wa madeni hayo.
“Serikali ya Awamu ya Tano haitakubali kuvunjika kwa ushirika na yeyote ambaye anadhani ushirika unaweza kufa anajidanganya,kama wamekula fedha watazitapika hadi fedha zote zipatikane’’,alisisitiza.
Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Ruvuma Bumi Masuba amesema Mkoa una vyama vya akiba na mikopo 124 ambapo kati ya vyama hivyo 38 vipo katika hatua ya kufutwa kufuatia agizo la serikali la kufuta vyama ambavyo havifanyi kazi na vimefunga ofisi zake kwa muda mrefu.
“Baadhi ya vyama hivyo vinakabiliwa na madeni lala ya nje kutokana na Taasisi mbalimbali za fedha kushindwa kurejesha madai ya wanachama ya kujitoa uanachama kwa sababu ya ukosefu wa fedha’’anasisitiza.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.