MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesikitishwa na kitendo cha Halmashauri ya Manispaa ya Songea kupata hati yenye mashaka na ameagiza wote waliosababisha wachukuliwe hatua.
Mndeme ametoa agizo hilo wakati anazungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kuhusu hoja na mapendekezo ya CAG kwa Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka 2018/2019.
Manispaa ya Songea imepata hati yenye mashaka kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo Mndeme amesema ripoti hiyo inasikitisha na kuumiza sana.
“Naagiza kuanzia sasa taratibu za kinidhamu zianze kuchukuliwa kwa wale wote waliosababisha Halmashauri ya Manispaa ya Songea kupata hati yenye mashaka,hatua zichukuliwe bila kujali awe ni Diwani au Mtendaji,suala hili limetutia aibu sana’’,alisisitiza Mndeme.
Mndeme ameagiza ufanyike uchunguzi ili kubainia wote walisababisha kupatikana kwa hati yenye mashaka kwa Halmashauri ya Manispaa ambayo ni kioo katika Mkoa wa Ruvuma na ina kila kitu ukilinganisha na Halmashauri nyingine za Mkoa.
Hata hivyo Mndeme amesisitiza kuwa kupata hati yenye shaka kuwafanye madiwani na watendaji waongeze bidii na kwamba CAG ametoa hoja na mapendekezo ambayo yanafikia idadi ya 54 kati ya hizo Hoja na Mapendekezo yaliyojibiwa na kufungwa ni 11 tu.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Hesabu za Serikali Deogratias Waijaha ameitaja sababu kuu iliyosababisha Halmashauri hiyo kupata Hati yenye mashaka kuwa ni kuripoti shilingi milioni 98 kwenye vitabu vyake vya Hesabu kama mapato ya ndani ambayo majibu yake hayakupatikana.
“Nawashauri kupitia vikao vyenu mfute milioni 98 kama mapato kwa sababu ile fedha itakwenda chanzo kikuu,haitarudi kwenu ,lakini taratibu za kijinai ziendelee kwa wote ambao walitenda hayo makosa kulingana na sheria za nchi,mlitakiwa kufanya mapema kabla ya kufunga Hesabu’’,alisisitiza Mkaguzi wa Hesabu za Nje.
Waijaha amesisitiza kuwa Manispaa ya Songea ilipata Hati yenye mashaka kwa tukio moja la udanganyifu wa milioni 98 na kwamba Manispaa hiyo haijapata hati chafu kwa sababu vitu vingine vyote vipo sawa.
Hata hivyo amesisitiza kuhakikisha wananunua vifaa kwa watu wenye risiti za mashine za EFD ili kuepuka kuendelea kuandikiwa hoja kutokana na kutumia watu ambao hawana risiti hizo hali ambayo inaikosesha serikali mapato .
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji kwa niaba ya Madiwani na watendaji ameahidi kufanyia kazi mara moja maagizo yote ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Licha ya kupata Hati yenye mashaka,Manispaa ya Songea katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019 imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 92 na kuweza kuchangia kwa asilimia 100 mfuko wa wanawake,vijana na wenye ulemavu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 191 mwaka 2018/2019.
Imeandika na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Mei 10,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.