KAMPUNI ya Mohamed Enterprise imetoa msaada wa vyakula na sabuni vilivyogharimu zaidi ya shilingi milioni 1.8 kwa vituo vitatu vya kulelea watoto yatima mjini Songea mkoani Ruvuma.
Mwakilishi wa Kampuni hiyo Angel Samasuba akizungumza mara baada ya kumaliza zoezi la ugawaji wa msaada huo,amevitaja vituo vya kulelea yatima vilivyopata msaada huo kuwa ni Kituo cha SWACCO kilichopo Kata ya Mwengemshindo,St.Anton cha Mfaranyaki na Kituo cha Mchungaji Mwema kilichopo Mjimwema.
Samasuba amesema Kampuni ya Mohamed katika vituo vyote vitatu imetoa jumla ya lita 120 za mafuta ya kula zilizogharimu shilingi 516,000 na mifuko ya unga wa sembe kilo 300 iliyogharimu shilingi 234,000.
Misaada mingine iliyotolewa ni sabuni za miche katoni 12 zenye thamani ya shilingi 120,000,vinywaji aina ya juisi katoni 30 zenye thamani ya shilingi 195,000 na mbuzi sita zenye thamani ya shilingi 600,000.
“Sisi kama Kampuni ya Mohamed Enterprise tumekuwa na kawaida ya kutoa misaada kwa makundi maalum na vituo vya kulelea watoto yatima kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali za kuwasaidia watu wenye uhitaji ili kuwafariji na kuwatia moyo’’,alisema Samasuba.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Mwakilishi wa kituo cha kulelea yatima cha Mchungaji mwema cha Mjimwema Sr.Maria Veronika OSB,ameishukuru Kampuni ya Mohamed kwa msaada huo ambao amesema utawasaidia watoto 39 ambao wanalelea na kituo hicho.
Naye Mwakilishi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha SWACCO Castrol Whero amesema kitendo kilichofanywa na Mohamed Enterprise kimeleta faraja kubwa kwa sababu yatima ni kundi maalum lililopo katika jamii linalohitaji msaada.
Amesema kituo cha SWACCO kilianza mwaka 2000 kikiwa na watoto 50 ambapo hivi sasa kituo hicho kinalea watoto 23 na watoto 31 wanahudumiwa wakiwa majumbani na walezi wao.
Vinsent Ndumbaro ni Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma akizungumza kwa niaba ya serikali,ameipongeza na kuishukuru Kampuni ya Mohamed Enterprise kuunga mkono juhudi za serikali za kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum ambapo ametoa rai kwa wadau wengine kuiga mfano huo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 5,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.