Serikali katika kutambua umuhimu wa afya bora kwa wananchi imeendelea kuweka kipaumbele katika huduma za afya zenye ubora na zinazowafikia wananchi popote walipo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu wa Mkoa wa Ruvuma Joel Mbewa wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, katika mkutano wa utambulisho wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii uliojumuisha viongozi wa mkoa, wilaya na halmashauri uliofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Mkoa, Songea (HOMSO) mjini Songea.
"Baada ya Serikali yetu kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na vitendea kazi na wataalam, sasa Serikali imekuja na mikakati maalumu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma na Elimu za afya huko huko walipo," alisema Mbewa.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia TAMISEMI inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutekeleza mikakati ya kuimarisha huduma za afya nchini ili kufikia huduma ya afya kwa wote ifikapo 2030.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mlezi wa Mkoa wa Ruvuma katika huduma za afya ngazi ya jamii, Mary Shadrack amesema kazi yao kubwa ni kuwajengea uwezo watoa huduma ngazi ya jamii wa mkoa, halmashauri na waliopo maeneo ya jamii.
Naye Afisa Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii, Bahati Mwailafu, akiiwakilisha Wizara ya Afya, amesema Mpango huo ulizinduliwa Januari 2024 ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza katika kutoa huduma hizo.
Hata hivyo Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Hilda Ndabalilo amesema anatambua ugumu wa majukumu wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii katika maeneo wanayoyaaimamia ya kutolea huduma hizo.
Ameongeza kuwa licha ya ugumu wa majukumu wanayotekeleza mchango wao hauwezi kubezwa kwani wamekuwa kiungo muhimu kati ya jamii na vituo vya kutolea huduma.
Watoa huduma za Afya ngazi ya jamii ni wananchi wa kawaida ambao wamepewa ujuzi, uhamasishaji na uelimishaji wa jamii lakini hutoa huduma ya kwanza kwa wagonjwa na Rufaa pale zinapohitajika.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.