MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,amemuagiza Kaimu Mkuu wa wilaya ya Nyasa Aziza Mangosongo kupitia kama ya ulinzi na usalama,kuwakamata na kuwafikisha mahakamani mafundi wa kampuni ya Emirate Builder Co Ltd waliohusika kuiba vifaa vya ujenzi wa miradi ya maji katika kijiji cha Lituhi na Liuli wilayani humo.
Kanal Laban ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti, wakati alipotembelea ujenzi wa miradi miwili ya maji katika kijiji cha Mwerampya na Liuli wilayani Nyasa inayotekelezwa na Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa).
Mkuu wa mkoa,amewataka wananchi kutambua kuwa miradi hiyo ni ya kwao,kwa hiyo wana wajibu wa kuilinda na kuepuka kununua vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi kutoka kwa mafundi.
Alisema,baadhi ya mafundi ndiyo wanaohusika kuiba vifaa na kuwaomba wananchi kutokuwa sehemu ya watu wanaohujumu miradi hiyo kwani Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kutatua changamoto na kuleta maendeleo.
“hakuna maana kama Mheshimiwa Rais Samia anaangaika usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi,alafu sisi ndiyo tunakuwa wa kwanza kuiba vifaa vinavyoletwa,tabia hii haikubailiki hata kidogo,nawaomba wananchi kushirikiana na serikali yenu kuwafichua watu wanaojihusisha na tabia hiyo”alisema Kanal Laban.
Aidha,amemtaka Mkandarasi kampuni ya Emirate Builders Co Ltd, kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwani wananchi wana hamu kubwa ya kupata maji safi na salama ili waweze kuyatumia katika shughuli zao za maendeleo.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nyasa Jeremia Maduhu alisema,Serikali imetoa Sh.bilioni 11,718,087.448 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya maji katika kijiji cha Lituhi na Liuli wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Maduhu alieleza kuwa, miradi yote miwili inajengwa na kampuni ya Emarate Builders Co Ltd na iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake huku akibainisha kuwa kati ya fedha hizo Sh.bilioni 6,595,019,723 zitatumika kutekeleza mradi wa maji Lituhi ambapo mkandarasi ameshalipwa shilingi milioni 989,252,958.50.
Kwa mujibu wa Maduhu,mradi huo utakapokamilika utahudumia vijiji saba vya Lituhi,Kihuru,Nkaya,Mwera mpya, Ndumbi Liweta na Mbaha vyenye takribani wakazi 26,477.
Alisema,katika mradi huo kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa tanki la la kuhifadhia maji la lenye mita za ujazo 500, kujenga vituo 19 vya kuchotea maji, ujenzi wa chanzo,ununuzi wa bomba za urefu wa mita 77.570,kuchimba mitaro na ujenzi wa ofisi ya chombo cha watumia maji.
Alitaja kazi zilizoanza kufanyika ni ujenzi wa chanzo, ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la lita 500,000 na ununuzi wa mabomba.
Akizungumzi mradi wa maji Liuli alisema,mradi huo umetengewa jumla ya Sh.bilioni 4,718,087,448 na utahudumia vijiji vitano vya Liuli,Nkalachi,Hongi,Puulu na Mkali A na B na utawanufaisha zaidi ya wakazi 25,808.
Baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa mradi huo ili kuwanusuru na adha ya kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Maria Ngailo mkazi wa kijiji cha Mwerampya kata ya Lituhi alisema,tatizo la maji katika kijiji hicho limesababisha hata baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo kwa kupata mimba wanapokwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.