Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametoa wito mzito kwa Maafisa Habari wote katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa wananchi wanapokea habari sahihi, kwa wakati na zenye tija kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali.
Akizungumza katika kikao kazi maalum kilichowakutanisha Maafisa Habari wa Mikoa, Halmashauri na Taasisi chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Jiji la Dodoma katika Mji wa Serikali Mtumba, Mhe. Mchengerwa alisisitiza kuwa nafasi ya Maafisa Habari ni ya msingi katika kupambana na upotoshaji.
“Msiwaache Watanzania walishwe habari potofu. Mmebeba dhamana kubwa ya kulinda ukweli. Iweni wazalendo kwa kazi yenu,” alieleza kwa msisitizo Waziri Mchengerwa.
Akiwaeleza umuhimu wa taaluma yao, Mchengerwa alisema Maafisa Habari ni rasilimali watu muhimu kwa maendeleo ya taifa, na akawahimiza kuwa wabunifu, waaminifu na wa kisasa katika kusambaza taarifa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
“Habari zenu ndizo zitakazoaminiwa na wananchi. Tujenge jamii inayotegemea taarifa rasmi, si uvumi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameelekeza kuwa Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri washiriki kikamilifu kwenye ziara za viongozi ili wawe na taarifa sahihi za kinachoendelea katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka waajiri wote kuhakikisha Maafisa Habari wanaokaimu nafasi za Ukuu wa Vitengo na wenye sifa stahiki, wanathibitishwa rasmi, ili waendelee kutekeleza vyema majukumu ya kuuhabarisha umma kuhusu mafanikio ya Serikali.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.