Mkuu wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Mheshimiwa Kapenjama Ndile, amewaonya wakulima wa mahindi katika wilaya hiyo kujiepusha na kuuza mazao yao kwa bei ya hasara kabla ya soko rasmi kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Julai. Ametoa wito huo kutokana na hali ya hewa isiyo ya kawaida iliyosababisha mahindi mengi kuharibika, hali inayoweza kudhoofisha ubora na thamani ya zao hilo muhimu kwa chakula na uchumi wa wananchi.
Akizungumza kwa msisitizo mkubwa, Mheshimiwa Ndile amesema mvua zilizoendelea kunyesha hadi wiki ya kwanza ya Mei zimeathiri uhifadhi wa mahindi, na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa mahindi mabovu. “Hata katika kununua, lazima tuwe na uchaguzi makini. Serikali haitapenda kununua mahindi yaliyochafuka, yaliyooza au yenye rangi zisizo za kawaida. Tunahitaji mahindi meupe, safi na bora,” amesisitiza.
Ameshauri sekta binafsi kuwekeza kwenye mashine za kisasa zinazoweza kupepeta na kuchambua mahindi kwa ubora unaohitajika, huku akiwahimiza wananchi kuwa wavumilivu na kutouza kwa haraka mazao yao kwa walanguzi wanaowapunguzia kipato. “Kama kuna shida ya pesa, wauze mazao mengine kama maharage, ufuta au soya. Lakini mahindi wayahifadhi, kwani ndiyo chakula kikuu na serikali italeta bei inayolipa,” amesema Ndile.
Kiongozi huyo ameonesha masikitiko kwa baadhi ya wakulima waliouza mahindi kwa bei ya chini mwaka jana kwa wafanyabiashara kutoka Kenya, kabla ya serikali kutangaza ununuzi rasmi kwa bei ya juu ya shilingi 700 kwa kilo. “Wananchi walikimbilia kuuza kwa Sh350, wengine Sh400. Mwezi mmoja baadaye serikali ikaanza kununua kwa Sh700. Wakaanza kulalamika ‘sikujua, sikujua.’ Hii ni fursa ya kujifunza,” amesema kwa ukali.
Kwa mara nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ameweka bayana kuwa serikali ipo tayari kuwanunulia wakulima mahindi kwa bei ya haki na ya ushindani kuanzia Julai mwaka huu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuinua kipato cha wakulima na kupunguza umasikini vijijini. “Tunasimama pamoja nanyi. Lakini ili mnufaike, mnatakiwa kuwa wavumilivu, wasikivu na wapangaji wa muda mrefu,” amehitimisha kwa matumaini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.