MBIO za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 zinatarajia kuanza mbio zake mkoani Ruvuma Aprili 8 mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea,leo ,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema Mwenge wa Uhuru Aprili 8 unatarajiwa kupokelewa katika kijiji cha Lituhi wilayani Nyasa ukitokea mkoani Njombe.
Brigedia Jenerali Ibuge amesema Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Ruvuma,utakimbizwa kilometa 1,052.3 ambapo unatarajiwa kutembelea miradi 62 yenye thamani ya Zaidi ya shilingi bilioni tano katika wilaya tano zenye Halmashauri nane.
Amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zinatarajia kukamilisha mbio zake Halmashauri ya Tunduru Aprili 15 na Aprili 16,Mwenge huo utakabidhiwa katika kijiji cha Lumesule mkoani Mtwara.
“Kama ilivyo jadi wana Ruvuma,naomba tujitokeze kwa wingi,kwa nderemo na vifijo katika maeneo yote ambayo Mwenge wa Uhuru utapita,pia kujitokeza katika maeneo ya mikesha’’,alisisitiza RC Ibuge.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewakumbusha wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kuvaa na kunawa mikono,sanjari ya kujitokeza katika zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19 ambalo litaendelea kutolewa katika maeneo yote ya mikesha.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 zimebeba ujumbe maalum usemao “Sensa ni msingi wa mipango ya maendeleo,shiriki kuhesabiwa,tuyafikie maendeleo ya Taifa’’.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Aprili 7,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.