Mwenge wa Uhuru 2024 umezindua jengo la kutolea huduma za dharura (EMD)katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambapo serikali imetoa Zaidi ya shilingi milioni 369 kutekeleza mradi huo.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chizza Marando amesema kati ya fedha zilizotumika shilingi milioni 300 zilitoka serikali kuu kupitia kwa wahisani (IMF) na Halmashauri ya Wilaya kupitia mapato ya ndani iliongeza Zaidi ya shilingi milioni 69.
Amesema mradi huo ulikamilika Aprili 2023 na ulianza kutoa huduma rasmi Juni 2023 ambapo hadi sasa jumla ya wateja 1,003 wamepatiwa huduma kupitia mradi huo.
“Faida za mradi huu ni Pamoja na kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ya kiafya,kupunguza rufaa za matibabu kwa wagonjwa na kupunguza gharama za rufaa kwa hospitali’’,alisema Marando.
Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo,Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Godfrey Mnzava amesema wamebaini dosari zilizojitokeza kwenye ukaguzi wa mradi huo hivyo amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Tunduru kufanya uchunguzi wa matumizi ya shilingi milioni 69 za nyongeza zilizotumika kwenye mradi huo bila utaratibu baada ya kuidhinishwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Tunduru.
Ameongeza kuwa wamebaini baadhi ya malipo katika utekelezaji wa mradi huo yamefanyika bila vocha yake kuwa na risiti ambapo ameagiza kuwepo na uthibitisho wenye risiti za kieletroniki.
Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru umepitia na kukagua miradi 11 yenye thamani ya shilingi bilioni 4.1
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.