Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ameitaka Mamlaka wa Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuvunja mkataba na Mkandarasi Kampuni ya Manyanya Enginnering Company Limited kutokana na Mkandarasi huyo kushindwa kukamilisha mradi wa jengo la abiria kwa wakati.
Naibu Waziri Kihenzile ametoa maagizo hayo Mkoani Ruvuma mara baada ya kukagua mradi huo na kutoridhishwa na maendeleo ya utakelezaji wake ambao ulitakiwa kuwa umekamilika mwishoni mwa mwaka 2023.
“Serikali imewekeza takribani bilioni 37 ili kuboresha miundombinu mbalimbali katika kiwanja hiki, na mkandarasi wa Jengo la abiria amelipwa muda mrefu fedha za kuanza mradi huu lakini amefanya kazi chache na kutelekeza mradi, hatuwezi kukubaliana na jambo hili ninawaelekeza TAA kuhakikisha mnapitia vipengele vyote vya mradi huu na mvunje mkataba huu maana ameshindwa kukamilisha kwa wakati’ amesema Naibu Waziri Kihenzile.
Naibu Waziri Kihenzile imeitaka TAA kuhakikisha Viwanja vya ndege vyote nchini vinapata hatia za umiliki ili kupunguza changamoto za uvamizi ambazo zimekuwa zikifanywa na wananchi wanaoishi pembezoni mwa viwanja hivyo.
Aidha Naibu Waziri Kihenzile ameipongeza TAA kwa kuendelea kuhakikisha utoaji wa huduma wa huduma katika viwanja vya ndege nchini unaboreshwa hali inayosababisha ongezeko la abiria, mizigo na mashirika ya ndege yanayotoa huduma katika viwanja nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile ameishukuru Serikali kwa kufanya maboresho katika kiwanja hicho kwani yamechochea kukua kwa uchumi wa mkoa huo sababu kukamilika kwake kumekuwa na ongezeko la usafirishaji wa mizigo hususani ya mboga mboga na matunda yanayozalishwa mkoani hapo.
Naye Meneja wa Kiwanja hicho Mhandisi Danstan Komba amesema kukamilika kwa ujenzi wa Barabara ya kuruka na kutua ndege (Run way), taa za kuongozea ndege, uzio, maegesho ya ndege, barabara ya kiungio (Taxing Way) na kituo cha nishati kumekifanya kiwanja hicho kuongeza wigo wa utoaji wa huduma ikiwemo kutumika kwa saa ishirini na nne (24).
Mhandisi Komba amemuhakikishia Naibu Waziri Kihenzile kuwa TAA itachukua hatua stahiki dhidi ya Mkandarasi huyo ili kuhakikisha mradi wa jengo la abiria unakamilika na kurahisisha utoaji wa huduma za abiria wanaotumia kiwanja hicho.
Katikati ni Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile akimsikiliza Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songea, Mhandisi Danstan Komba (kushoto), kuhusu maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika cha Ndege cha Songea, wakati Naibu Waziri huyo alipokagua Kiwanja cha Ndege
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.