HIFADHI ya Gesimasowa yenye ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya 760 ambayo ipo katika Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ni miongoni mwa vivutio adimu vya utalii ambavyo havifahamiki na wengi.
Hifadhi hiyo ilianzishwa kama msitu wa hifadhi mwaka 1975 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa wakati huo, Hayati Dkt.Lawrence Gama.
Mwaka 2015,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma katika kipindi hicho hayati Said Mwambungu alisimamia mchakato wa kupandisha hadhi msitu huo na kuwa hifadhi.
Moja ya vivutio vilivyopo katika hifadhi hii ni mapumziko ya ndege maarufu duniani anayeitwa tandawili machaka (Derhams) wenye uwezo wa kuruka toka bara moja hadi bara jingine,ndege hao wanazaliana katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo iliyopo Makete mkoani Njombe.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha kuwa utafiti umebaini kuwa ndege hao wanapumzika ndani ya hifadhi hiyo kwa miezi kadhaa kisha wanaendelea na safari kupitia Bonde la ufa hadi ziwa Nyasa hatimaye wanasafiri hadi nchini Afrika ya Kusini na mabara mengine ya Ulaya na Amerika.
Kulingana na Challe,hifadhi ya Gesimasowa ni mapito ya ndege hao ambao wanatoka Kaskazini mwa Afrika kuelekea Afrika ya Kusini ambao wanafuata milima ya Livingstone iliyopo ziwa Nyasa na kwamba ndege hao pia wanapumzika Mwambao mwa ziwa Nyasa ambako kuna mazingira ambayo yanavutia ndege hao kuishi.
Hata hivyo Challe anasema,Hifadhi ya Gesimasowa pia ina mfumo wa ikolojia wa pori la Selous ambalo sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa kuwa hifadhi hiyo ni mapitio ya wanyamapori wanaotoka katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kuelekea Bonde la ziwa Nyasa kupitia pori la Liparamba hadi Hifadhi ya Niasa nchini Msumbiji na kurudi tena Tanzania.
Anawataja wanyama ambao unaweza kuwaona katika hifadhi ya Gesimasowa kuwa ni tembo, simba,ndege, nyati, pofu na samaki adimu duniani aina ya mbelele na mbasa.
Challe anabainisha zaidi kuwa Hifadhi ya Gesimasowa ni maingiliano ya mito miwili ya Hanga na Lutukira katika Halmashauri ya Madaba ambayo inatengeneza mto Ruhuhu unaomwaga maji yake ziwa Nyasa.
Anasema Mto Ruhuhu ndiyo mazalia ya samaki aina ya mbelele na mbasa ambao katika duniani nzima wanapatikana ziwa Nyasa pekee.
“Utafiti umebaini Samaki aina ya mbelele na mbasa ni adimu,wanapatikana ziwa Nyasa pekee na wanazaliana katika mto Ruhuhu ambao unachangia asilimia 20 ya maji katika ziwa Nyasa’’,anasema Challe.
Utafiti kuhusu Samaki hao katika mto Ruhuhu na ziwa Nyasa ulifanywa na Mtafiti Fransis Challe mwaka 2010 ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kitivo cha Sayansi,Teknolojia na Mazingira na chapisho la utafiti huo lilitolewa mwaka 2011.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa wavuvi katika ziwa Nyasa wanafanya uharibifu wa mazingira katika eneo la Folkland Lituhi kwenye maingiliano ya mto Ruhuhu na ziwa Nyasa hivyo wanaharibu vifaranga wa samaki ambao wanaingia katika ziwa Nyasa.
Challe anasisitiza eneo la maingiliano ya mto Hanga na Mto Lutukira ndani ya Hifadhi ya Gesimasowa linatakiwa kulindwa na kuhifadhiwa kwa sababu Samaki aina ya mbasa na mbelele wanazaliana kwenye Maingilio ya mito hiyo,kisha wanasafiri hadi ziwa Nyasa na kuendelea na Maisha.
Anasema wakati wa kuzaliana samaki hao wanarudi tena kwenye maingilio ya Mto Hanga na Mto Lutukira,hivyo hifadhi ya Gesimasowa ni eneo muhimu kitaifa na kimataifa katika Uhifadhi na utalii kwa kuwa ndiyo eneo pekee duniani ambako Samaki jamii ya mbasa na mbelele wanazaliana.
Hata hivyo anasema hifadhi ya Gesimasowa,bado ni mpya na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa maliasili zilizopo katika hifadhi hiyo zinalindwa ili ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kulingana na sheria ya wanyamapori namba tatu ya mwaka 2009 wananchi hawaruhusu kufanya shughuli zozote ndani ya hifadhi hizo,hivi sasa wanyamapori wanahama toka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,wakipitia hifadhi ya Gesimasowa,hifadhi ya Litumbandyosi, Pori la Liparamba na kuvuka mpaka hadi hifadhi ya Niassa nchini Msumbiji.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anasema ana utaja Mkoa wa Ruvuma kuwa una fursa nyingi za utalii wa kitamaduni na ikolojia.
Anavitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa ni hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Pori la akiba Liparamba,Mto Ruvuma,Ziwa Nyasa,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, hifadhi ya Mwambesi,Jiwe la Mbuji,hifadhi ya Ruhila,hifadhi ya Gesimasowa na vivutio vingine vingi.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Februari 8,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.