Katika eneo la Migelegele wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma sasa kunasikika kelele za matumaini na ndoto mpya kupitia Sekondari ya Wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Shule hiyo ya kisasa iliyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 4.5 imejengwa na serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwa kimbilio la elimu bora kwa watoto wa kike, imeibuka kama nguzo ya mabadiliko makubwa kwa jamii inayozunguka. Wasichana zaidi ya 400 kutoka familia za kipato cha chini sasa wanapata elimu katika mazingira rafiki yenye mabweni, maabara za kisasa, na walimu waliobobea.
Tangu kuanzishwa kwake, shule hiyo imevuka matarajio kwa matokeo ya kitaaluma, ikichagiza ongezeko la ufaulu wa masomo ya sayansi. Mbali na mafanikio ya kitaaluma, Sekondari ya Dkt. Samia imekuwa kitovu cha mafunzo ya uongozi, maadili, na stadi za maisha, ikiandaa wasichana wenye ujasiri wa kushindana kitaifa na kimataifa. Wazazi na viongozi wa eneo hilo wanasema shule hiyo si tu mradi wa elimu, bali ni dira ya matumaini kwa vizazi vijavyo.
Kwa jina lake na dhamira yake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameacha alama isiyofutika katika moyo wa elimu ya mtoto wa kike. Ndani ya wilaya ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ambako ndoto zilikuwa zimezimika, sasa kuna mwanga unaong’aa kwa kila msichana anayekanyaga lango la shule hiyo.
Sekondari hii siyo tu jengo, bali ni chombo cha mapinduzi ya kijamii ikiandika upya historia ya elimu ya wasichana mkoani Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.