Benki ya NMB imetoa madawati 150 yenye thamani ya shilingi milioni 16.5 kwa shule tatu za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Shule ambazo zimepatiwa madawati hayo ni Shule ya Msingi Matimira, Magagura na Magima, ambapo kila shule imepata madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5,500,000.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Mtela Mwampamba, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama Ndile wakati wa makabidhiano ya madawati hayo yaliyofanyika katika shule ya msingi Matimira, ameishukuru benki ya NMB kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kupunguza kero ya upungufu wa madawati kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo.
Naye Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Roman Degeleki, amesema benki ya NMB ni wadau wa elimu wanaotambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia za kusimamia upatikanaji wa huduma bora za Elimu hivyo wana wajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali ili kuboresha sekta hiyo.
Ameeleza kuwa changamoto za sekta ya Elimu kwa benki ya NMB ni jambo la kipaumbele, na walipopata maombi ya kuchangia maendeleo ya elimu katika shule hiyo walifarijika kwa kuwa sekta ya Elimu ndio chachu ya maendeleo katika jamii.
Ameongeza kuwa benki ya NMB imekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida kwa jamii akibainisha kwa zaidi ya miaka nane mfululizo wamekuwa wakitenga asilimia 1 ya faida kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayowazunguka.
Akisoma taarifa ya shule ya msingi Matimira, Mwalimu Renista Vungu, amesema shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa madawati, kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi, ambao kwa sasa wapo 810.
Kwa mujibu wa Mwalimu Vungu, shule hiyo ilikuwa na mahitaji ya madawati 256, huku yaliyokuwepo yakiwa 190 pekee, hivyo kulikuwa na upungufu wa madawati 66, ambapo kupitia ufadhili wa benki ya NMB, shule imepokea madawati 50, hatua ambayo itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mhe. Menans Komba, amewataka walimu wa shule hizo kusimamia ipasavyo matumizi ya madawati ili yaweze kudumu kwa muda mrefu akiwasihi wanafunzi kuyalinda na kuepuka kuyaathiri kwa namna yoyote, kwani yamepatikana kwa lengo la kuwasaidia katika safari yao ya elimu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.