ENEO la Masonya lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma lina utajiri wa utalii wa malikale na utambulisho wa Taifa ambalo bado halifahamiki na wengi.
Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 100 lina vivutio adimu vya utalii wa malikale ikiwemo nyumba yenye namba A 10 ambayo walikuwa wanafikia na kuishi Marais Hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Hayati Samaro Machel wa Msumbiji kuanzia 1966 wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema viongozi hao pia wakiwa katika nyumba hiyo walitumia kibanda maalum kilichopo jirani ya nyumba hiyo kama chumba cha mawasiliano na nchi zilizokuwa katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.
“Kutoka nyumba ya viongozi hao hadi kibanda cha mawasiliano lilijengwa handaki la chini kwa chini ambalo lipo hadi sasa lilokuwa linatumiwa na viongozi hao wa kitaifa’’anasema Nyamusya.
Eneo la malikale la Masonya lenye ukubwa wa ekari 100 lipo kilometa 12 kaskazini mwa mji wa Tunduru na kwamba eneo hili linatakiwa kuendelezwa kwa sababu linaweza kutoa mchango mkubwa katika nyanja za utalii,uchumi,elimu na utafiti.
Hata hivyo serikali hivi sasa inalitumia eneo la malikale la Masonya kwa shughuli za kielimu ambapo katika eneo hili imejenga shule ya sekondari ya Masonya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Masonya Elice Banda anaitaja mikakati ya awali ya uhifadhi wa malikale ya Masonya kuwa ni hifadhi hiyo kutumika kwa shughuli za kielimu na kujengwa kwa mnara wa kumbukumbu.
Hata hivyo Mkuu huyo wa shule anasema katika kudumisha kumbukumbu ya historian a mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika,Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliamua kuweka alama za kudumu kwa kujuenga mnara wa kumbukumbu.
“Majina ya wapiganaji wote waliokufa wakati wa harakati hizo yameandikwa,hii dhahiri kuwa kituo hiki daima kitatukumbusha watanzania na watoto wetu,majukumu yetu na vizazi vingine vijavyo vitaona mchango wa Tanzania katika harakati za Bara la Afrika’’,anasisitiza Banda.
Historia inaonesha kuwa kabla ya mwaka 1966,eneo la malikale la Masonya lilikuwa ni msitu ambapo katika mwaka huo ndipo serikali iliwapokea watu kutoka nchini Msumbiji na kuwakabidhi eneo hilo katika kipindi chote cha kupigania uhuru nchini Msumbiji toka katika utawala wa Mreno.
Erick Soko ni Afisa Elimu Msaidizi Makumbusho ya Taifa ya Majimaji anasema tangu tangu wakabidhiwe eneo hilo la Masonya watu wa Msumbiji mwaka 1966,wamewahi kutembelea na kuishi kadhaa viongozi mashuhuri akiwemo Hayati Samora Machel ambaye alifika mara kadhaa wakati wa harakati za kupigania uhuru.
Soko anabainisha zaidi kuwa katika kipindi cha miaka kumi kuanzia 1966 hadi wanawake toka nchini Msumbiji wameishi katika eneo la Masonya na kwamba Umoja wa Wanawake wa Msumbiji uliojulikana kwa OMM ulianzia Masonya mwaka 1973.
“Mwaka 1975 baada ya uhuru wa Msumbiji kutangazwa ndipo kambi ya Masonya ilivunjwa na wanamsumbiji walirejea katika nchi yao,tangu mwaka 1975 hadi mwaka 1989 eneo hili lilibaki bila matumizi’’,anasisitiza Soko.
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mwaka 1990 ilianza kuliendeleza eneo la Masonya kwa matumizi ya kielimu ilianzishwa shule ya sekondari ya Masonya kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Tunduru(TETFU) ambapo mwaka 1991 hadi 1993 walitenga fedha ili kuboresha miundombinu iliyoachwa na watu wa Msumbiji na kuongeza majengo ya shule.
Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Masonya Elice Banda anasema mwaka 1994 usajiri wa wanafunzi wa kidato cha kwanza ulianza ambapo hadi kufikia mwaka 2016 shule hiyo ina wanafunzi wa kuanzia kidato cha kwanza hadi sita.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 5,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.