Na Albano Midelo
WANANCHI wa Mkoa wa Ruvuma wanaendelea kunufaika na uongozi wa serikali ya Awamu ya Sita ambapo katika kipindi cha mwaka 2022/2023 serikali ilitenga bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 28.7 kutekeleza miradi ya maji mkoani Ruvuma.
Meneja wa Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga anasema hadi sasa serikali imeleta zaidi ya shilingi bilioni 19 kutekeleza miradi hiyo katika wilaya za Songea,Mbinga,Nyasa,Namtumbo na Tunduru.
Anasema katika kipindi cha mwaka 2023/2024 serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 26.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji mkoani Ruvuma.
Anaitaja baadhi ya miradi iliyoidhinishiwa fedha wilayani Mbinga kuwa ni mradi wa maji Linda milioni 450,mradi wa maji Tukuzi milioni 450,mradi wa maji Mtama milioni 400,mradi wa maji Kipololo milioni 400,mradi wa maji Kigonsera milioni 300 na mradi wa maji Ngima milioni 253.
Katika Wilaya ya Songea miradi iliyoidhinishiwa fedha anaitaja kuwa ni mradi wa maji Lwangeni milioni 618,mradi wa maji Lipaya bilioni 1.9,mradi wa maji Lipokela milioni 734.74,mradi wa maji Kizuka milioni 730.4,mradi wa maji Mtyangimbole bilioni 5.56 na mradi wa maji Ndelenyuma bilioni 1.6.
Meneja huyo wa maji Mkoa wa Ruvuma anaitaja baadhi ya miradi ya maji katika Wilaya ya Nyasa kuwa ni ukarabati wa mradi wa maji Ng’ombo shilingi milioni 130,ukarabati wa mradi wa maji Lunyele milioni 280,mradi wa maji Mbuyula-Ndengele shilingi milioni 649.86 na mradi wa maji Mitomoni milioni 944.
Mhandisi Ganshonga anaitaja miradi ya maji iliyoidhinishiwa fedha katika kipindi cha mwaka 2023/2024 wilayani Namtumbo kuwa ni mradi wa maji Naikesi milioni 179.5,mradi wa maji Likusanguse milioni 300,mradi wa maji Mchomoro milioni 320.14 na mradi wa maji Msisima milioni 168.
Miradi ya maji katika wilaya ya Tunduru anaitaja kuwa ni mradi wa maji Namwinyu milioni 535,mradi wa maji Hulia milioni 300,mradi wa maji Tuwemacho milioni 150,mradi wa maji Msinji milioni 200,Mradi wa maji Msechela milioni 200,mradi wa maji Nakapanya milioni 150 na mradi wa maji Masonya milioni 94.95.
“Utekelezaji wa miradi hiyo umeongeza huduma za upatikanaji wa maji kutoka asilimia 58.4 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 70 mwaka 2023,kuongeza huduma ya maji kutoka watu 891,616 mwaka 2018 hadi kufikia watu 1,035,325 mwaka 2023’’,anasema Ganshonga.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anasema asilimia 70 ya watu wanaoishi vijijini mkoani Ruvuma ambao ni 1,294,156 kulingana na sensa ya watu ya mwaka 2022 wanapata huduma ya maji safi na salama ambapo lengo la Mkoa ni kufikia asilimia 85 kupata maji safi na salama kwa wakazi wa vijijini ifikapo mwaka 2025.
Kanali Thomas anabainisha kuwa Rais Dkt.Samia ameongeza idadi ya vijiji vyenye huduma ya maji kufikia 366 kati ya vijiji 533 vilivyopo Mkoani Ruvuma.
Kanali Laban anasisitiza kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwatua ndoo kichwani wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na kwamba hadi kufikia Juni 30,2023 Mkoa wa Ruvuma ulikuwa unatekeleza jumla ya miradi 33 ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni zaidi ya bilioni 55.
Naye Mhandisi wa Maji Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles anampongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 11.2 katika Wilaya hiyo ili kutekeleza miradi sita ya maji katika kipindi cha mwaka 2023/2024.
Stella Mhagama Mkazi wa Kijiji cha Lipaya wilayani Songea anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi wa maji ambapo anasema kwa miaka mingi wanawake na Watoto wamekuwa wanapata kero ya kusafiri umbali mrefu kufuata maji mtoni na kubeba kichwani.
Diwani wa Kata ya Mpitimbi wilayani Songea Mheshimiwa Issa Kindamba anampongeza Rais Dkt.Samia kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza mradi wa maji Lipaya ambao anasema unakwenda kupunguza umbali wa wananchi kutembea kufuata maji na kupunguza magonjwa yanayosambazwa na maji yasiyo salama.
Romanus Ndunguru Mkazi wa Kijiji cha Utili wilayani Mbinga anaishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwajengea mradi wa maji Utiri kwa gharama ya shilingi milioni 428 ambao umekamilika kwa asilimia 99 na unakwenda kuhudumia watu 3,626.
Anania Nkomola Mkazi wa Kijiji ch Hinga wilayani Nyasa kwa niaba ya wananchi wenzake anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea mradi mkubwa wa maji Ngumbo wenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 ambao tayari wananchi wameanza kunufaika nao.
Wananchi wa Kata ya Liuli wanamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza mradi wa maji katika Kijiji cha Hongi Kata ya Liuli wilayani Nyasa ambao umegharimu shilingi bilioni 4.7 ambapo hadi sasa mradi umeanza kuwahudumia wananchi.
Mrad mwingine mkubwa wa maji wilayani Nyasa ni ule ambao unatekelezwa katika kijiji cha Mwerampya kata ya Lituhi unaogharimu shilingi bilioni 6.5 ambapo tayari baadhi ya vijiji vimeanza kunufaika na mradi huo.
Nao wakazi wa Misechela wilayani Tunduru akiwemo Amina Mohamed na Mariam Hussein wanaishukuru serikali kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji ya bomba wenye thamani ya shilingi bilioni tatu ambapo wananchi hivi sasa wanapata huduma ya maji katika visima vinavyotumia pampu za mkono.
Hakuna ubishi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla moja ya vitu ambavyo watamkumbuka Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni namna anavyoshughulikia kwa ufanisi wa hali ya juu changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijijini na mijini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.