Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma imepokea jumla ya Shilingi bilioni 11.974 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza kwenye kikao cha wakurugenzi wa Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika mjini Mbinga,Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Mbinga Bi.Amina Seif alisema fedha zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta za elimu, afya, maendeleo ya jamii, kilimo, utawala, biashara na mifugo.
“Tuna kila sababu ya kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema Bi. Amina.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Halmashauri hiyo katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilipokea jumla ya shilingi bilioni 5.6, mwaka 2022/2023 ilipokea bilioni 5.4 na mwaka 2023/2024 Halmashauri hiyo imepokea shilingi Milioni 974.6.
Amebainisha zaidi kuwa katika sekta ya elimu pekee,kwa kipindi cha miaka mitatu Halmashauri hiyo imepokea shilingi bilioni 7.8 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu.
Ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika sekta ya elimu kuwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa 182 , Ujenzi wa shule mpya nne ambazo amezitaja kuwa ni sekondari ya Lusonga, shule ya msingi Kipika, shule msingi Mpepai na shule ya sekondari Matarawe.
Kulingana na Mkurugenzi huyo katika sekta ya Afya kwa kipindi cha miaka mitatu Halmashauri imepokea shilingi bilioni 2 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo viwili vya afya vya Mbangamao na Myangayanga na ujenzi wa zahanati tisa.
Amebainisha zaidi kuwa katika kipindi hicho kwenye sekta ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri imepokea shilingi bilioni 2.64 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhawilishaji fedha katika kaya maskini na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.