MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ametoa miezi mitatu kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa umma vinafungwa mifumo ya kukusanya mapato (GOTHOMIS).
Brigedia Jenerali Ibuge ametoa agizo hilo wakati anafungua kikoa cha mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya kwa viongozi wa serikali kutoka Halmashauri na wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Mkuu wa Mkoa ametoa agizo hilo kutokana na vituo vingi vya serikali kukosa mifumo ya kukusanya mapato (GOTHOMIS) ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya vituo 280 vya kutolea huduma za afya vilivyopo mkoani Ruvuma,ni vituo kumi tu ndivyo vimefungwa mifumo hiyo.
“Kufikia Septemba Mosi,2021,vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa umma,viwe vimefungwa mifumo ya GOTHOMIS bila kukosa,Septemba 2,2021,niwe nimepata taarifa ya utekelezaji na baada ya hapo,ukaguzi wa kushitukiza utaendelea na kuchukua hatua’’,amesisitiza RC Ibuge.
Mkuu wa Mkoa pia amewaagiza wakuu wa Wilaya na wakurugenzi katika Halmashauri zote,kuhakikisha mapato na matumizi ya vyanzo vyote katika Halmashauri yanajadiliwa kwenye vikao vya kisheria na amekitaja moja ya kigezo kitakachotumika kuangalia ufanisi wa ukusanyaji mapato katika Mkoa wa Ruvuma katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 ni lazima kufikia zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya vyanzo vya sekta ya afya.
RC Ibuge ameziagiza Halmashauri zote kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya kwa umma vinatuma kila mwezi kwa wakati madai ya huduma iliyotolewa kwa wanachama wa Mfuko wa Afya Jamii ulioboreshwa(iCHF) na Mfuko waTaifa wa Bima ya Afya(NHIF).
Kutokana na asilimia ndogo ya wananchi waliojiunga na (iCHF) mkoani Ruvuma,RC Ibuge ameziagiza Halmashauri zote kufanya uhamasishaji mkubwa wa jamii kujiunga na mfuko huo ambapo hadi sasa Mkoa umeandikisha kaya zilizohai 11,820 sawa na asilimia 3.3 wakati lengo ni kufikia kaya 180,085 sawa na asilimia 50.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Kanga ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa,ikiwemo kuongeza ukusanyaji mapato kupitia mfumo wa GOTHOMIS na kuongeza uhamasishaji kwa jamii kujiunga na (iCHF).
Dr.Kanga amesema mfuko wa iCHF mkoani Ruvuma ulianza kutekelezwa mwaka 2019,ambapo kitaifa Mkoa ulishika nafasi ya mwisho ambapo hivi sasa Mkoa umepanda hadi kufikia nafasi ya 11 kitaifa na kwamba kikao kazi hicho kitaongeza ufanisi na tija.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 11,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.