Mkuu wa mkoa Ruvuma Chistina Mndeme amewaagiza wakuu wa Taasisi serikalini kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuanzia ngazi ya chini.
Mndeme ametoa kauli hiyo katika kikao cha kazi cha watendaji na wakuu wote wa Taasisi za serikali mkoani Ruvuma kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa Songea.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa nimekuwa nikipokea kero mbalimbali ambazo wakati mwingine kero hizo zingetatuliwa katika ngazi ya wilaya au kijiji,nimeona ni vema niwaite wakuu wa Taasisi zote, kwa sababu tunapaswa kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yetu’’,alisisitiza.
Amewaagiza watendaji hao kusikiliza kero za wananchi kwa wakati na kuwaagiza kutosubiri kero kuwafikia ofisini badala yake waweke ratiba ya kwenda kwa wananchi kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Mndeme ameagiza kila Halmashauri na Taasisi kuunda mkakati wake wa kushughulikia kero za wananchi ili kupunguza kero hizo kuanzia ngazi ya chini.
“Sasa hivi tuna tatizo la mara kwa mara la kukatika kwa umeme,wewe Meneja wa TANESCO kazi yako ni nini,watu wamelipia umeme,hawajaunganishiwa umeme,wewe kama Meneja wa TANESCO kwanini huendei kwa wananchi na kutoa sababu za kero hizo,tutoe taarifa kwanini maji yamekatika,sio mimi Mkuu wa Mkoa nikatoe taarifa kwa wananchi,tuwasiliane na wananchi’’, alisema Mndeme.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amezitaja sababu mbili kubwa zinaosababisha kero kwa wananchi ni kutokufanyika vikao vya kisheria na wananchi na kutokuwepo kwa mahusiano mazuri miongoni mwa watendaji wa serikali hivyo ameagiza kufanyika kwa vikao vya kisheria na kuimarisha mahusiano ndani ya Taasisi za serikali ambayo yatasaidia kupunguza kero kwa wananchi.
“Tukitekeleza majukumu yetu vizuri kwa wananchi,tutaifanya kazi ya Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuwa nyepesi,sisi ndiyo tupo chini,tutoke maofisini,tusisubiri ziara ya Mkuu wa Mkoa,ninyi wakuu wa Taasisi mnaruhusiwa kwenda kuzungumza na wananchi na kutatua kero zao’’,alisisitiza.
Mndeme ameagiza kila Taasisi kuandaa rejesta ya malalamiko ya ambayo itaratibu malalmiko pia kuunda timu ndogo itakayosaidia kuratibu malalamiko na kuyafikisha kwa mkuu wa Taasisi na kwamba kero za kisera zipelekwe ngazi ya juu ili ziweze kupata utatuzi wa kisera.
Ili kuhakikisha utatuzi wa kero unakuwa endelevu,Mkuu wa Mkoa ameziagiza Taasisi za serikali kila mwisho wa mwezi kufanya tathimini namna kero zilivyoshughulikiwa na kutoa taarifa za kero zinazohitaji ufafanuzi wa kisera kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amesema ilani ya CCM ya 2020/ 2025 inalitaja moja ya jukumu lake ni kusikiliza malalamiko ya wananchi hivyo jambo linalofanywa na uongozi wa mkoa wa Ruvuma ni utekeleza wa ilani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema katika kushughulikia malalamiko ya wananchi na kwamba hakuna mfumo wa pamoja,hali inayosababisha wananchi kutojua wakimbilie wapi katika kupata suluhu ya matatizo yao.
Ili kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,Mkoa wa Ruvuma umeazimia kuunda timu ya Mkoa ya kutatua kero zinazowakabili wananchi ambayo itakutana kila baada ya miezi mitatu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 15,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.