Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewahakikishia usalama wanafunzi wa kidato cha Sita wawapo shuleni hususani katika kipindi hiki kigumu cha kupambana na janga la Corona.
Akizungumza na wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Kigonsera iliyopo Wilaya ya Mbinga,Mndeme amesema,Mkoa wa Ruvuma hauna Mgonjwa hata mmoja wa Corona,hata hivyo ametoa rai kwa wanafunzi kuendelea kuchukua tahadhari ya kukabiliana na maambukizi ikiwemo kutumia barokoa,maji na sabuni.
Mndeme amewataka wanafunzi kuongeza bidii na kasi ya kusoma , kutii maelekezo watakayopewa na walimu wao, ili mwaka huu Mkoa wa Ruvuma katika Matokeo ya kidato cha Sita iwe miongoni mwa Mikoa mitatu itakayofanya vizuri Kitaifa.
“Shule ya Kigonsera ina historia iliyotukuka kitaifa kwa sababu imemtoa Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa,pia imemtoa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa hiyo shule hii ina heshima yake’’,alisisitiza.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewaagiza TARURA kutatua changamoto ya Barabara inayofika shuleni hapo ili itengenezwe na kupitika mwaka mzima kipindi cha kiangazi na Masika.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Kigonsera Ponsiano Ngunguru amewataja wanafunzi wa Kidato cha sita walioripoti shuleni ni 163 na ambao bado hawajaripoti hadi kufikia Juni 2 mwaka huu ni 199 na kwamba shule hiyo ina jumla ya wanafunzi wa kidato cha sita 362.
Shule ya Sekondari ya Kigonsera ni miongoni mwa shule kongwe za Serikali nchini iliyoanzishwa mwaka 1938.
Wakati huo huo Mkuu wa shule ya sekondari ya Maposeni Dismas Nchimbi amewataja wanafunzi wa kidato cha sita walioripoti katika shule hiyo hadi kufikia Juni 3 kuwa ni 191 kati yao wavulana 101 na wasichana 90 .Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 222.
Imeandikwa na Aneth Ndonde
Kutoka Ofisi ya Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 3, 2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.