Na Albano Midelo,Namtumbo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesikitishwa na hali isiyoridhisha ya malezi na uangalizi wa mtoto.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia ambayo kimkoa yamefanyika Kijiji cha Suluti wilayani Namtumbo,amesema wazazi na walezi wengi wamekuwa hawatimizi ipasavyo majukumu ya malezi na kusababisha malezi ya upande mmoja.
“Takwimu kutoka ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2023 zinaonesha kuwa jumla ya mashauri 3,441 yalipokelewa na kushughulikiwa ambapo mashauri 1,611 sawa na asilimia 47 yalihusu matunzo ya watoto,mashauri 831 sawa na asilimia 24 yalihusu matatizo ya ndoa na mashauri 969 sawa na asilimia 29 yalihusu mashauri nje ya ndoa’’,alisema Kanali Abbas.
Amebainisha kuwa Ofisi ya Ustawi wa Jamii imekuwa ikipokea kesi za matunzo ya Watoto na malalamiko yanayoelekezwa upande wa akinababa.
Ametoa rai kwa wazazi na walezi ambao wamefarakana kutambua kuwa mtoto bado anastahili malezi yaliyo bora hivyo ni vema kuweka mpango mzuri wa kumlea mtoto ili asiathirike kimalezi na kwamba wazazi wajitahidi kuvumiliana ili kuepusha kuachana kusiko kwa lazima hivyo kumuathiri mtoto.
Akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia Mariam Juma ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameitaja kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema tukubali tofauti zetu kwenye familia,kuimarisha malezi ya Watoto, inawakumbusha wazazi na walezi kuweka kando tofauti zao na kuangalia malezi na huduma zinazostahili kwenye familia.
Juma amebainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2023 mashauri 2,859 ya ukatili yalitolewa taarifa na kushughulikiwa katika ofisi za ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma na kwamba mashauri 121 yalifikishwa mahakamani.
Hata hivyo amesema mashauri 77 sawa na asilimia 63.6 yalihukumiwa,kati ya mashauri 1,580 ya Watoto,mashauri 1050 sawa na asilimia 66.6 yaliwahusu wasichana wakati mashauri 1,279 ya watu wazima,mashauri 1,030 sawa asilimia 80.5 yaliwahusu wanawake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya amesema wazazi wote wawili wanatakiwa kuwajibika kwa malezi ya familia ili fahari ya mtoto na mafanikio yake yawe kwa wazazi wote wawili kwa kuwa mtoto ni wa wazazi wote.
Amewashauri wazazi na walezi kuwalea Watoto kwa misingi inayompendekeza Mwenyezi Mungu na kuheshimu sheria za nchi,
Hata hivyo Malenya amesisitiza upendo kwa familia ambao unafanikisha malezi bora kwa familia na kutahadharisha kuwa wazazi na walezi wasipoungana kwa dhamira hawataweza kutimiza ndoto za Watoto wao.
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa Mei 20,1993 lilitenga siku maalum ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia lengo likiwa ni kutambua nafasi ya familia katika jamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.