Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amezindua rasmi kituo cha mabasi cha Lundusi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mradi uliotekelezwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) awamu ya pili kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Lundusi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kanali Ahmed ameeleza kuwa TASAF ni nyenzo muhimu ya kupambana na umaskini kwa kuwa inawawezesha wananchi kutumia fursa za kuinua hali zao za kiuchumi.
“Awamu ya pili ya utekelezaji wa mpango wa TASAF umejikita sana katika masuala ya kuwezesha kaya kutumia fursa za kukuza uchumi na kuongeza kipato katika kaya za walengwa, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu, maji safi na salama pamoja na miundombinu ya kukuza uchumi katika ngazi ya jamii,” alisema Kanali Ahmed.
Ameeleza kuwa ujenzi wa kituo cha mabasi pamoja na maduka ya biashara katika eneo hilo ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla, hivyo ametoa wito kwa viongozi na wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa manufaa kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya halmashauri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bwana Shedrack Mziray, amesema TASAF ilitoa shilingi milioni 686.3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha mabasi baada ya kupokea maombi kupitia halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mwaka 2001, TASAF imekuwa ikitoa ruzuku kwa halmashauri zote nchini kwa lengo la kuwawezesha walengwa, na hadi kufikia sasa, jumla ya shilingi trilioni 1.17 zimetolewa na kuwafikia walengwa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, amesema kuwa mkoa utaendelea kushirikiana kwa karibu na TASAF ili kuhakikisha miradi iliyobaki inakamilika kwa wakati, huku wakiendelea kuratibu na kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa huduma za miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na uwekezaji huo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.