MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua Mpango wa Usafirishaji wa Dharura kwa akinamama wajawazito,waliojifungua na Watoto wachanga (m-mama).
Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya Rufaa ya Mkoa mjini Songea,Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Mkoa Jumanne Mwamnkoo amesema mfumo huo utahakikisha vituo vya kutolea huduma za afya na wenye dharura wanapata usafiri wa dharura utakaopatikana wakati wote.
Amesema hadi sasa jumla ya madereva 140 kutoka katika Mkoa wa Ruvuma wametambuliwa, kuchaguliwa na kupata mafunzo maalum ya mfumo wa m-mama na kwamba wapo tayari kufanya kazi hiyo.
“Madereva hao watahusika kutoa huduma za usafiri wa dharura pale tu magari yetu ya kubeba wagonjwa yanapokosekana kwa sababu mbalimbali zinazoeleweka,muhimu ni kuhakikisha kila mama mwenye dharura anafikishwa sehemu stahiki ili aweze kupata huduma bora kwa wakati’’,alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Kanali Thomas amesema mfumo huo ulizinduliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Aprili 6,2022 ambapo hadi sasa zaidi ya mikoa 19 nchini imekwishaanza kutekeleza mfumo wa m-mama ambapo Mkoa wa Ruvuma unaanza sasa kutekeleza mfumo huo ili kuboresha moja ya lengo kuu la Afya ya Huduma ya rufaa ya mama na mtoto.
Mkuu wa Mkoa amewaagiza wakurugenzi kutekeleza mfumo huo katika Halmashauri zote,kuhakikisha kila mwaka bajeti ya usafiri wa dharura kwa wajawazito na Watoto wachanga inaingizwa katika mipango ya vituo vya kutolea huduma za afya na kufanya tathmini ya mahitaji ya vituo vyote vinavyotoa huduma za afya katika Mkoa.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Hilda Ndambalilo amesema Mkoa umepiga hatua katika kupunguza vifo vya akinamama vitokavyo na uzazi kutoka vifo 31 mwaka 2020 hadi kufikia vifo 22 mwaka 2022.
Ndambalilo amesema vifo vya Watoto pia vimepungua kutoka vifo 326 mwaka 2020 hadi kufikia vifo 271 mwaka 2022 ambapo amesisitiza hatua mbalimbali kuendelea kuchukuliwa ili kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto.
Amesema Mkoa umedhamiria kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana ikiwa ni Pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya za dharura za upasuaji kutoka vituo vya huduma 31 hivi sasa hadi kufikia vituo 35 ifikapo mwaka 2024.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Chihoma Mhako amesema Mkoa una magari 13 ya kubeba wagonjwa yanayofanya kazi ambayo yanatoa huduma za dharura kwa wagonjwa ambapo mahitaji ya Mkoa ni magari 38 hivyo Mkoa bado unakabiliwa na upungufu mkubwa kwenye usafiri wa dharura.
Amesema kwa mwaka 2022 kulikuwa na jumla ya rufaa za dharura 1,306 za wajawazito zilizofanyika na kwamba zipo rufaa ambazo hazikupata mafanikio kutokana na kuchelewa kufika katika kituo cha huduma za dharura kwa wakati.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Dr.Edson Fransis amesema kuzinduliwa kwa mfumo wa m-mama,serikali imedhamiria kuokoa Maisha ya mama na mtoto na kwamba mradi utawezesha mama mjamzito,aliyejifungua na Watoto kupata huduma za haraka.
Amebainisha kuwa mgonjwa aanapobainika kuwa na tatizo atapiga simu ambayo itapokelewa na mtaalam katika hospitali ya Mkoa na kupata maelekezo ya kituo cha dharura cha Kwenda ili kupata huduma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.