Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas anatarajia kuzindua uwekaji wanyamapori kwenye kisiwa cha Lundo ziwa Nyasa Novemba 5 mwaka huu.
Hafla ya uwekaji wanyamapori jamii ya swala na ndege inatarajia kushirikisha wadau mbalimbali wa utalii ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa pia anatarajia kukabidhi rasmi hifadhi ya Mbambabay kwa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Mkuu wa Mshauri wa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema wanatarajia kuanzisha hifadhi ya Mbambabay ambayo inajumuisha visiwa vya Lundo,Mbambabay na milima ya Mbamba,Tumbi na Ndengere wilayani Nyasa.
Challe anaitaja hifadhi ya Mbambabay itakuwa na ukubwa wa eneo la hekta 597 na kwamba maeneo hayo yanafaa kwa kufuga wanyamapori na ndege.
Hata hivyo anasema Kati ya hekta hizo, mlima Mbamba una eneo lenye ukubwa wa hekta40,mlima Tumbi hekta 110,kisiwa Mbambabay chenye hekta 27,kitakuwa maalum kwa ufugaji wa ndege na kisiwa cha Lundo chenye ukubwa wa hekta 20,kitawekwa wanyamapori jamii ya swala na ndege..
“Milima na visiwa hivi vimejaaliwa kuwa na uoto mzuri wa miombo,mawe yanayozunguka visiwa hivi na milima kando kando ya ziwa yana hifadhi samaki adimu wa mapambo zaidi ya aina 400’’,anasisitiza Challe.
Kwa mujibu wa Challe,eneo la hifadhi ya Mbambabay ni muhimu sana kwa upande wa Tanzania hususan katika matumizi ya shughuli za utalii kama vile utalii wa kuvua samaki,kupiga mbizi,kuogelea,utalii wa kuendesha mitumbwi na kuweka kambi kwenye fukwe.
Mtalaam huyo wa uhifadhi anasema eneo hilo likihifadhiwa litatumika kwa ajili ya mazalia ya samaki na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi wanaotegemea shughuli za uvuvi.
Mbambabay ikihifadhiwa inaweza kuleta ushindani kibiashara hapa nchini kwa sababu katika nchi yetu hakuna eneo linaloweza kutoa mchanganyiko mzuri wa huduma za kitalii kama zitakazotolewa katika eneo hili.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.