Mkoa wa Ruvuma unatarajia kulima jumla ya hekta 1,006,325 za mazao ya chakula,biashara na mazao ya bustani katika msimu wa mwaka 2023/2024 ambazo zinatarajia kutoa mavuno ya tani 2,168,041.
Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Ngao amesema kati ya hekta hizo,mazao ya chakula ni hekta 642,906 zinazotarajia kutoa mavuno ya tani 1,882,473.
Amesema mazao ya biashara zinatarajia kulimwa hekta 348,441 zinazotarajia kutoa mavuno ya tani 100,557 na mazao ya bustani jumla ya hekta 14,978 zitalimwa na zinatarajia kutoa mavuno ya tani 185,012.
“Mkoa umelenga kuongeza uzalishaji wa zao la parachichi kutoka tani 1,768 zinazozalishwa sasa hadi kufikia tani 37,500 ifikapo mwaka 2025’’,alisema Ngao.
Hata hivyo amesema kampuni mbalimbali zimeonesha nia ya kununua parachichi katika Mkoa wa Ruvuma na kwamba zao hilo ni fursa kwa wakulima kwa kuwa mahitaji ya ndani na nje ya nchi ni makubwa.
Akizungumzia kuhusu zao la kahawa Afisa Kilimo huyo wa Mkoa wa Ruvuma amesema Mkoa unatarajia kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kutoka tani 23,355 hivi sasa hadi kufikia tani 55,000 ifikapo mwaka 2025.
Kuhusu zao la soya Ngao amesema Mkoa umelenga kuongeza uzalishaji wa soya kutoka tani 5,510 kwa msimu wa 2022/2023 hadi kufikia tani 10,000 kwa msimu 2023/2024 na kwamba Mkoa unaendelea kuwahamasisha wananchi kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Kulingana na Afisa Kilimo huyo,katika msimu wa mwaka 2023/2024 Mkoa wa Ruvuma umelenga kuongeza uzalishaji katika zao la korosho kutoka tani 28,014 hadi kufikia tani 29,135 na kwamba uzalishaji wa zao la ufuta pia unatarajia kuongezeka kutoka tani 9,649 hadi kufikia tani 112,061.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa pembejeo za kilimo,Afisa Kilimo huyo amesema katika msimu wa mwaka 2023/2024 kuanzia Julai 2023 hadi Januari 2024 zimeingizwa jumla ya tani 90,000 za pembejeo za kilimo na kusambazwa kwa wakulima kiasi cha tani 62,540,225 kati ya mahitaji ya tani 112,692.
Amesema hadi sasa tani 27,459,775 zinapatikana katika maghala ya Kampuni na kwenye maduka ya mawakala mkoani Ruvuma.
Baadhi ya wakulima mkoani Ruvuma wamemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka ruzuku kwenye mbolea ambayo imempunguzia mkulima mzigo wa gharama za mbolea kwa asilimia 50 hali iliyosababisha wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya hekta 4,007,746 zinazofaa kwa kilimo ambapo hadi sasa eneo ambalo linalimwa ni wastani wa hekta 897,171 sawa na asilimia 22 ya eneo lote ambalo linafanya Mkoa kuwa ziada ya hekta 3,110,575 sawa na asilimia 78.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.