WADAU wa kilimo na Ushirika kutoka wilaya zote mkoani Ruvuma wamekubaliana kuwa hakuna soya wala ufuta utakaonunuliwa na kutoka nje ya Mkoa wa Ruvuma bila kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Wamepitisha azimio hilo katika mkutano wa uendeshaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge na kufanyika Ikulu Ndogo mjini Songea.
Mkutano huo umewashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya,makatibu tawala,wakurugenzi wa Halmashauri, wenyeviti wa Halmashauri,Mstahiki Meya,viongozi wa vyama vikuu vya ushirika vya SONAMCU na TAMCU,Mwakilishi kutoka Bodi ya Leseni ya stakabadhi ghalani,maafisa kilimo na watumishi wengine.
“Tumekubaliana wote kwenye kikao hiki,hivyo mkasimamie,hakuna soya wala ufuta utakaonunuliwa kutoka nje ya Mkoa bila kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani’’,amesisitiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
RC Ibuge ameziagiza Halmashauri na wilaya zote mkoani Ruvuma kusimamia kikamilifu utekelezaji huo na kuongeza kuwa Halmashauri zina jukumu la kuunda na kuhuisha Kamati za usimamizi wa stakabadhi ghalani ili kutatua changamoto ndogo ndogo za wadau.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pia ameagiza elimu endelevu kuhusu taratibu,sheria na miongozo iliyopo katika mfumo wa stakabadhi ghalani ianze kutolewa kila Halmashauri na kwamba vyama vya ushirika vinahusika zaidi ili wadau wapate uelewe wa kina kuhusu umuhimu wa mfumo huo.
Mfumo wa stakabadhi ghalani katika mazao ya soya na ufuta mkoani Ruvuma,umekuwa msaada katika kuwapatia wakulima kipato kikubwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa msimu wa mwaka 2018/2019 kiasi cha tani 2,855.38 za soya na tani 8,428.27 za ufuta ziliuzwa kupitia mfumo huo na kwamba mwaka 2019/2020 tani 1,499.8 za soya na tani 12,234.76 za ufuta ziliuzwa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea wanaodaiwa kufanya udanganyifu kuwa sehemu ya ubadhirifu wa kuandika stakabadhi, kuingiza kwenye mfumo wa mapato na kibali.
RC Ibuge amewataja watumishi hao kuwa ni Noel Chengula,Mbaya Kitete na Hamisi Mwanaupanga ambapo Mkuu wa Mkoa amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma kuwasimamisha kazi ili wapishe taratibu za kisheria.
Mkuu wa Mkoa pia amemwagiza Mkuu wa TAKUKURU kufanya uchunguzi wa haraka ili suala hilo likamilike kisheria,huku akimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma kufanya ukaguzi katika mfumo wa mapato katika Mkoa na kuwasilisha taarifa kwake Julai 30 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pia amewaagiza wakuu wa Wilaya na Kamati za Usalama kufanya kazi ya kufuatilia upotevu wa mapato ya ndani katika Halmashauri zao na kupeleka taarifa kwake Juni 30 mwaka huu.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewapongeza wafanyabiashara wa mazao mkoani Ruvuma kupitia chama chao cha Umoja wa Wanunuzi wa Mazao Vijijini Mkoa wa Ruvuma (UWAMAVIRU) kuwafichua watumishi wasio kuwa waaminifu na ambao wanatumia vituo vya ukaguzi wa mazao kwa maslahi yao binafsi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 26,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.