RUVUMA WAADHIMISHA KUZALIWA KWA RAIS SAMIA KWA KUPANDA MITI
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaongoza wananchi kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kupanda miti katika shule za Msingi na sekondari Mashujaa Manispaa ya Songea.
Akizungumza mara baada ya kukamilisha zoezi hilo,Kanali Laban amesema Mkoa umeamua kuifanya shughuli ya kupanda miti ya matunda ikiwa ni maalum kuunga mkono siku ya kuzaliwa kwa Rais.
“Nichukue fursa hii kumtakia heri na afya tele Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anaposherehekea siku yake ya kuzaliwa,kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma tunampongeza sana,Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda ili aendelea kuliongoza Taifa letu la Tanzania’’,alisema
Amesema mara nyingi Rais Dkt.Samia amekuwa wanahimiza watanzania kupanda miti ya matunda hivyo katika tukio hilo ,Kanali Thomas ameongoza kupanda miti ya matunda aina ya miparachichi na mipera katika shule za msingi Mashujaa na shule ya sekondari Mashujaa.
“Jambo muhimu sio tu kupanda miti,bali kuhifadhi na kuilinda ili miti hiyo iweze kukua,miti hii kwa kuwa ni ya matunda inaweza kutumika kama chakula kwa wanafunzi hivyo kujenga afya za wanafunzi na wal’mu’’,alisema RC Thomas.
Mkuu wa Mkoa amewahimiza wananchi wote mkoani Ruvuma kuendelea kupanda miti nyumbani na kwenye mashamba ambapo amesema mashamba mengi ya kahawa hivi sasa yamebakia vipara baada ya miti kukatwa hivyo amewashauri wakulima kuhakikisha mashamba yao yanapandwa miti.
Amesema uzinduzi wa Kampeni ya wiki ya upandaji miti kimkoa ilifanyika Januari Mosi mwaka huu ambapo jumla ya miti milioni 1.1 ilipandwa ambapo amesema zoezi la upandaji miti ni endelevu hadi mvua zitakapoishia.
Afisa Maliasili Mkoa wa Ruvuma Africanus amesema kwenye zoezi hilo maalum lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa jumla ya miti 400 imepandwa kati ya hiyo miti ya matunda 200 na miti ya kupanda kwenye mipaka 200.
Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2023 unatarajia kupanda miti ya aina mbalimbali zaidi ya milioni nane ambayo inapandwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Taasisi za Serikali, Taasisi binafsi na wananchi.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Januari 27,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.