Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi za mwaka 2022 zinaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma una jumla ya wajane wapatao 49,702.
Hayo yasemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Rehema Madenge wakati anafungua maadhimisho ya siku ya wajane Duniani ambayo katika Mkoa wa Ruvuma yamefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Hata hivyo amesema takwimu za kitaifa za Sensa ya watu na makazi zinaonesha kuwa Tanzania ina wajane 1,396,262 na kwamba wajane wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Baadhi ya wajane pia hujikuta wanafukuzwa nyumbani mwao,kutengwa na kunyanyaswa na ndugu wa mume Pamoja na jamii na wengine hulazimishwa kuolewa na ndugu wa marehemu pasipo ridhaa yao,pia wajane wengine hukosa utetezi mbele ya vyombo vya sheria wanapotafuta haki zao’’,alisisitiza Madenge.
Akizungumzia kaulimbiu ya siku ya wajane ya mwaka huu inayosema,Imarisha mifumo ya upatikanaji wa nishati ,kukuza uchumi wa wajane na familia,Madenge amesema kaulimbiu hiyo inasisitiza na kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Amesema Tanzania kama yalivyo mataifa mengine inatekeleza jitihada za jamii kutumia nishati safi ili kuondokana na uharibifu wa mazingira na athari za kiafya.
Hata hivyo Katibu Tawala huyo amesisitiza kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inawatambua na kuwajali wajane ambapo serikali imekuwa inafanya juhudi mbalimbali kuhakikisha changamoto za wajane zinatatuliwa.
Awali risala ya wajane iliyosomwa kwenye maadhimisho hayo imeipongeza serikali kwa kutambua siku hiyo muhimu ambayo inatoa fursa kwa wajane kutafakari mipango ,mikakati,mafanikio na changamoto ili kuimarisha na kuzitatua.
Wameipongeza serikali kwa kutoa fursa ya mikopo inayotokana na asilimia nne ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajane kiuchumi ambapo hadi sasa vikundi vitatu vya wanawake wajane katika Manispaa ya Songea vimepatiwa shilingi milioni 5.3.
Maadhimisho ya kilele cha siku ya wajane Duniani hufanyika kila mwaka Juni 23 ambapo kwa Mkoa wa Ruvuma yamefanyika Juni 24,2024
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.