WANANCHI wa kijiji cha Namasakata Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,wamelalamikia gharama kubwa za upatikanaji wa maji ya bomba kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta yanayotumika kuendeshea nishati ya umeme wa Jenereta kupeleka maji kwenye makazi yao.
Wameiomba Serikali kupitia shirika la umeme Tanzania(Tanesco), kuharakisha ujenzi wa mradi wa umeme vijijini(Rea) ili waweze kuondokana na kadhia hiyo ambayo imesababisha baadhi yao kushindwa kumudu gharama licha ya Serikali kukamilisha ujenzi wa wa maji.
Asha Pendeka alisema,Serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira Ruwasa umefanya kazi kubwa ya kujenga mradi na kufikisha huduma ya maji katika makazi yao,lakini wanashindwa kutumia maji hayo kwa sababu ya gharama kubwa ambapo bei kwa ndoo ya lita 20 ni Sh.100 na ndogo ya lita 10 ni Sh.50 fedha ambazo ni nyingi ikilinganisha na hali halisi ya vipato vyao.
Diwani wa kata ya Namasakata Rashid Usanye alisema, mradi huo wameupokea vizuri na huduma inapatikana wakati wote,hata hivyo tatizo kubwa kwa wanufaika wa mradi huo ni gharama kubwa kutokana na matumizi ya Jenereta kuendesha mradi huo.
Alisema, kwa wiki moja wanatumia takribani Sh.100,000 hadi 150,000 fedha za kununulia mafuta ya Disel kujaza maji kwenye tenki la lita 60 na ameiomba Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini(Tanesco)kuharakisha kufikisha umeme katika kijiji hicho ili uweze kuendesha mashine zinazotumika kusukuma maji kutoka kwenye chanzo kwenda kwenye tenki.
Alisema, umeme ukipatikana hata gharama ya maji itapungua na wananchi wataweza kumudu gharama za maji na pia utasaidia kuharakisha shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.
Kaimu Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira wilaya ya Tunduru Kassim Dinny alisema, mradi huo umekamilika ambapo unahudumia wakazi wapatao 3,898 na umetekelezwa kwa gharama ya Sh.152,113,475.00.
Alisema,kati ya fedha hizo Serikali kuu imetoa Sh.147,154,975.00,mchango wa wananchi Sh.4,958,500.00 na fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi za mradi huo kwa mujibu wa mkataba zimetumika.
Aidha alisema, kwa kuwa mradi umejengwa kwa kuwatumia mafundi wa ndani badala ya mkandarasi wamefanikiwa kuokoa Sh.8,216,339.50 ambazo zimetumika kutekeleza kazi za nyongeza ambazo ni kuongeza mtandao wa bomba urefu wa mita 1,723 na kujenga vituo vinne vingine vya kuchotea maji.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.