SEKONDARI ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyojengwa katika kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma kwa gharama ya shilingi bilioni nne imeanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano.
Mkuu wa Shule hiyo Mwl.Dafrosa Chilumba amesema ili kutekeleza mradi wa ujenzi wa sekondari hiyo serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika awamu ya kwanza ilitoa shilingi bilioni tatu.
Ameyataja majengo ambayo yalijengwa katika awamu ya kwanza ya ujenzi ulianza Aprili 2022 kuwa ni ujenzi wa jengo moja la utawala,madarasa 12 na maabara nne za Jiografia,Kemia,Fizikia na Biolojia.
Majengo mengine ameyataja kuwa ni nyumba mbili za walimu zenye uwezo wa kuchukua familia tatu,mabweni Matano yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 kila bweni,mfumo wa maji safi wenye matanki mawili na mitaro yenye urefu wa mita 1050,vyoo matundu 16,bwalo kubwa la chakula,chumba cha jenereta,njia za kutembea na uzio.
Hata hivyo amesema utekelezaji wa ujenzi katika awamu ya kwanza umefikia zaidi ya asilimia 95 na kwamba serikali imeleta shilingi bilioni 1.1 kuanza kutekeleza mradi kwa awamu ya pili.
Ameitaja miundombinu ambayo inajengwa katika awamu ya pili kuwa ni ujenzi wa madarasa kumi,nyumba mbili za walimu zenye uwezo wa kuchukua familia nne,jengo la TEHAMA, maktaba,mabweni manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kila moja.
“Wanafunzi wa kidato cha tano ambao tumepangiwa na serikali kuanza masomo ni 249 wengi wameshafika,wanafunzi hao wanasoma michepuo mitano ,wanafunzi wanafurahia mazingira ya kuvutia yenye huduma zote muhimu,walimu wapo wa kutosha,hakuna mwanafunzi anayewaza kuhama’’,alisisitiza.
Stella Magaho ni Mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika sekondari ya Wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan mchepuo wa PCB amesema wanafunzi walioripoti katika shule hiyo wanafurahia mazingira rafiki ya kusoma na kwamba hakuna changamoto yoyote .
Mwanafunzi huyo ambaye ni Kiranja Mkuu kwa niaba ya wenzake anaishukuru serikali kwa kuwajengea sekondari bora kwa Watoto wa kike ambapo ameahidi watafanya vizuri katika masomo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema sekondari ya wasichana ya Namtumbo ni miongoni wa sekondari mpya 11 ambazo Rais Dkt.Samia ametoa zaidi ya shilingi bilioni 7.7. kujenga sekondari hizo mkoani Ruvuma katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Kanali Thomas amezitaja shule hizo mpya kuwa zimejengwa katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma na kwamba shule zimejengwa kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP).
Hata hivyo amesema katika Halmashauri ya Tunduru zimejengwa shule tatu za sekondari kupitia mradi wa SEQUIP na kwamba katika Halmashari ya Namtumbo pia zimejengwa shule mbili ikiwemo shule ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Deogratias Ndejembi amesema serikali ya Awamu ya sita katika mwaka 2022/2023 imetoa zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari 176 za kata kupitia program ya SEUIP.
“Fedha hizo zimetolewa kujenga shule za sekondari za kata katika kata zisizo na shule na kata zenye wanafunzi wengi zaidi ukilinganisha na miundombinu ya shule zilizopo’’,alisisitiza Ndejembi.
Hata hivyo amesema katika Mkoa wa Ruvuma kupitia program hiyo mwaka huu,serikali imetoa shilingi bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya saba za sekondari za kata.
Sekondari ya wasichana ya Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyopo Namtumbo mkoani Ruvuma ni miongoni mwa sekondari kumi mpya za wasichana za mikoa zilizojengwa na serikali ya Awamu ya Sita.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.